Nigeria yafungwa na Ugiriki

Nigeria ikishangilia bao dhidi ya Ugiriki, Kombe la Dunia
Image caption Joseph Yobo, (kushoto), Peter Odemwingie, (katikati), na Danny Shittu, (kulia )wakishangilia bao la Nigeria lililofungwa na Uche Kalu dhidi ya Ugiriki.

Nigeria ilipoteza mechi yake ya pili kwenye michuano ya Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini baada ya kushindwa na Ugiriki mabo 2-1 katika uwanja wa Free State mjini Bloemfontein.

Kitu pekee kinachoiwezesha Nigeria kubakia katika mashindano ni kuhakikisha inapata ushindi mkubwa kwenye mchuano wao dhidi ya Korea Kusini Jumanne wiki ijayo, na pia kutumainia kwamba Argentina nao watawashinda Ugiriki kwa mabao mengi.

Katika mechi ya mapema siku ya Alhamisi Argentina ilikuwa timu ya kwanza kufuzu kwa raundi ya pili baada ya kuifunga Korea Kusini mabao 4-1.

Nigeria ndiyo iliyotangulia kufunga dakika ya 16 kupitia mpira wa adhabu, uliosukumwa hadi wavuni na Uche Kalu.

Katika dakika ya 44 kiungo wa Ugiriki Dimitrios Salpingidis alisawazisha kufuatia kizaaza kwenye lango la Nigeria.

Mlinda lango wa Nigeria ambaye ndiye aliyepigiwa kura kuwa mchezaji bora wa mechi aliponyokwa na mpira dakika ya 71 baada ya mashambulio ya Ugiriki, na hapo mlinzi Vasileios Torosidis akafunga bao la pili na la ushindi kwa Ugiriki.

Nigeria walibaki na wachezaji 10 tangu dakika ya 14 baada ya Sani Kaita kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumpiga teke kijinga mlinzi wa Ugiriki Vasileios Torosidis.

Pia mlinzi Taye Taiwo alipata jeraha, akalazimika kupumzika na nafasi yake kutawaliwa na Uwa Echiejile, ambaye pia alijeruhiwa na nafasi yake kujazwa na Rabiu Afolabi.