Serbia yaiangusha Ujerumani

Miroslav Klose
Image caption Miroslav Klose akionyeshwa kadi ya pili ya njano

Serbia iliifunga Ujerumani bao 1-0 mjini Port Elizabeth na kuweka wazi nafasi za kufuzu kwa raundi ya pili ya Kombe la Dunia kwa timu za kundi D.

Katika mechi ya ufunguzi, Ujerumani ilikuwa imeifunga Australia mabao 4-0 na kujiwekea matumaini makubwa ya kuvuka kwa urahisi kutoka kundi D ambalo pia linajumuisha Ghana.

Lakini kiungo wa kati wa Serbia Milan Ivanovic alibadilisha mtazamo huo kwa bao la dakika ya 35 lililoiwezesha timu yake kuzoa pointi tatu.

Udhaifu wa Ujerumani ulianza katika dakika ya 30 baada ya refa kutoka Uhispania Alberto Undiano Mallenco kumuonyesha kadi ya pili ya njano mshambuliaji Miroslav Klose, na hivyo Ujerumani kubaki na wachezaji 10.

Lukas Podoski alipoteza nafasi ya kusawazisha baada ya mkwaju wake wa penalti kuokolewa na kipa wa Serbia Vladimir Stojkovic katika kipindi cha pili.

Matokeo hayo yana maana kwamba Ujerumani, Serbia na Ghana zina pointi 3 kila mmoja, na Australia ambayo itacheza na Ghana siku ya Jumamosi haina pointi yoyote.

Itawalazimu Ghana kujitahidi kuishinda Australia ili kujipa matumaini makubwa ya kufuzu kwa raundi ya pili, kwa kuwa Ujerumani inawasubiri kwa mchuano wa mwisho wa makundi, mechi inayoaminika itakuwa ngumu sana.

Ghana iliishinda Serbia katika mechi ya ufunguzi, na Ujerumani inafahamu kwamba ili kufuzu kwa raundi ya pili lazima waishinde Ghana jumatano wiki ijayo.