Raia wa Australia hawaonekani Afrika

Wasiwasi unazidi kuongezeka juu ya usalama wa wakurugenzi wa migodi ambao ni raia wa Australia kutokana na ndege yao kutokujulikana ilipo.

Ndege hiyo ilikuwa ikitokea Cameroon kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Abiria tisa walikuwepo kwenye ndege hiyo, akiwemo mmoja wa matajiri wakubwa wa Australia Ken Talbot.

Kundi hilo lilitoka katika mji mkuu wa Cameroon, Yaounde siku ya Jumamosi kutembelea miradi ya madini ya chuma huko Yangadou, eneo lililo kijijini huko Kongo.

Image caption Ken Talbot, tajiri mkubwa Australia, ambaye naye hajulikani alipo

Jeshi la Cameroon linaongoza msako wa ardhini na angani kwenye msitu mkubwa sana.

Ndege waliyokuwa wakisafiria lilikodishwa na kampuni ya migodi ya Australia, Sundance Resources.

Eneo walilotembelea ni pamoja na mradi wa Mbalam linalosambaa mpaka Cameroon na Congo, ambapo Sundance Resources lina matumaini ya kupata tani milioni 35 ya madini ya chuma kwa mwaka.

Shirika la habari la AFP limemnukuu waziri wa mambo ya nje wa Australia Stephen Smith akisema, " Tuna wasiwasi mkubwa juu ya usalama wao."

Sundance Resources imesema baada ya kuripotiwa kuwa ndege haikutua siku ya Jumamosi jitihada zake zimelenga kusaidiana na mamlaka za Cameroon, Congo na nchi jirani ya Gabon.

Taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo imesema " Shughuli zote zimesimamishwa, huku raslimali zote zikielekezwa kwenye jitihada za msako na uokozi."

Msemaji wa ofisi ya wizara ya mambo ya nje ya Uingereza amesema wafanyakazi wa Cameroon walikuwa wanajaribu kutambua nani alikuwa kwenye ndege hiyo, baada ya mashirika ya habari kuripoti kuwa Waingereza wawili walikuwa miongoni mwa abiria hao.

"Tumepata taarifa hizo na tunafanya uchunguzi. Wafanyakazi wetu wa ubalozini wamekuwa wakiwasiliana na balozi ndogo ya Australia."