Marekani yamwita Jenerali juu ya makala

Jenerali Stanley McChrystal
Image caption Jenerali Stanley McChrystal

Kamanda mkuu wa majeshi ya Marekani nchini Afghanistan ameitwa nyumbani Washington baada ya kuchapishwa kwenye makala ya jarida moja ambalo lilimnukuu yeye na washauri wake wakiwakosoa maafisa na wanadiplomasia waandamizi wa uongozi wa Obama.

Jenerali Stanley McChrystal ameomba radhi kwa makala hayo yaliyochapishwa katika jarida la Rolling Stone.

Katika makala hayo Jenerali McChrystal ananukuliwa akisema anahisi amesalitiwa na balozi wa Marekani mjini Kabul Karl Eikenberry.

Washauri wa jenerali huyo wanamkejeli makamu wa Rais Joe Biden na kusema wamevunjwa moyo na Rais Barack Obama.

Afisa wa Ikulu ya Marekani alisema Jenerali McChrystal aliamrishwa kuhudhuria binafsi mkutano wa kila mwezi kuhusu Afghanistan na Pakistan badala kupitia njia ya simu.

Msemaji wa halmashauri kuu ya utawala wa majeshi ya Marekani, Adimeri Mike Mullen alisema alizungumza kwa simu na Jenerali McChrystal kuelezea masikitiko yake.

Makala hayo ya The Rolling Stone yenye wasifu wa Jenerali McChrystal iliyokuwa na kichwa cha habari "The Runaway General" yaani jenerali mtoro iliyoandikwa na mwandishi wa habari aliyepewa fursa ya kuandamana na kamanda huyo na wasaidizi wake, yamepangwa kuchapishwa siku ya Ijumaa.

Jenerali McChrystal amejaribu kujikosha katika taarifa yake ya Jumanne kwa kusema " Naomba samahani kwa wasifu huu. Ilikuwa ni makosa makubwa ambayo hayastahili kutokea."