Wapiga kura wapuuza vitisho Somaliland

Rais wa Somaliland Dahir Riyale Kahin
Image caption Rais wa Somaliland Dahir Riyale Kahin

Wengi wamejitokeza katika uchaguzi wa Rais huko Somaliland, licha ya kutolewa vitisho na wanamgambo.

Waangalizi wa kimataifa wamesema watu wamesimama kwenye foleni ndefu katika vituo mbalimbali vya kupigia kura kwenye jimbo hilo lililojitenga.

Serikali hiyo imefunga mipaka ya nchi yake kwa kuhofia wanamgambo kutoka jirani yao Somalia wangeweza kuvuruga uchaguzi huo.

Wanamgambo hao wa kundi la al-Shabab waliwaonya wapiga kura kubaki nyumbani.

Mapema wiki hii, kundi hilo lilitoa ujumbe kupitia redio, likielezea uchaguzi huo wa kidemokrasia kama "kanuni za shetani".

Matumaini ya kutambuliwa

Serikali ya Somaliland iliwaomba wapiga kura kupuuza onyo hilo.

Somaliland ilijitenga na Somalia mwaka 1991 na haitambuliwi kimataifa kama taifa huru.

Image caption Wafuasi wa chama kikuu cha upinzani Kulmiye

Mchambuzi wa BBC Martin Plaut amesema eneo kubwa lina amani na lina utawala thabit, ukilinganisha na eneo kubwa lililobaki huko Somalia.

Amesema watu wengi Somaliland wana matumaini kuwa uchaguzi huu ukifanyika kwa salama, itaongeza nguvu katika hoja yao ya kutaka iwe huru.

Idadi kubwa ya waangalizi wa kimataifa wako eneo hilo kuangalia uchaguzi ho.

Rais aliye madarakani Dahir Riyale Kahin anapambana na wapinzani wawili:Ahmed Mohamed Silaanyi kutoka chama kikuu cha upinzani, Kulmiye, na kiongozi wa chama cha Justice and Welfare, Faisal Ali Warabe.

Matokeo yanatarajiwa kutangazwa katika kipindi cha wiki moja.