Teknolojia ya goli yazua mjadala

Frank Lampard wa England
Image caption Frank Lampard akiwa ametaharuki baada ya kukataliwa goli lake wakati wa mechi ya timu yake ya England dhidi ya Ujerumani

Shirikisho la soka dunia FIFA limekataa kuzungumzia uwezekano wa kukubali kutumia teknolojia inayowezesha marefa kubaini ikiwa mpira umevuka mstari wa golini au la.

Mjadala kuhusu haja ya kutumika kwa teknolojia hiyo ulichacha siku ya Jumapili wakati wa mechi ya Kombe la Dunia kati ya Ujerumani na England, ambapo kiungo wa England Frank Lampard alikataliwa bao , licha ya mpira kuonekana wazi ukiwa umevuka mstari wa golini.

Baada ya kupata ushindi wa mabao 4-1 na kufuzu kwa robo fainali, Ujerumani sasa inasubiri kukutana na Argentina ambayo iliifunga Mexico mabao 2-1 na kujiandikishia nafasi miongoni mwa nane bora.

Mchuano kati ya Argentina na Mexico pia ulichochea mjadala kuhusu teknolojia ya kubaini goli, baada ya Carloz Tevez kuifungia Argentina bao la kwanza , akionekana ameotea.

Lakini katika mkutano wa kila siku na waandishi wa habari kwenye Kombe la Dunia huko Afrika Kusini, msemaji wa FIFA Nicolas Maingot alisema pahali pa kujadiliwa swala hilo sio kwenye Kombe la Dunia.

Alisema uamuzi wa kutotumiwa kwa teknolojia hiyo uliafikiwa na bodi ya kimataifa ya vyama vya soka ambayo pia inashirikisha FIFA na Uingereza, na kwa hivyo hakuna uwezekano wa kubadilisha uamuzi huo.

Image caption Sepp Blatter, FIFA

Maingot pia aliongeza kusema FIFA haitaruhusu matukio ya uwanjani yenye utata kurudiwa kwenye skrini kubwa zinazowekwa ndani ya viwanja kama ilivyofanyika kufuatia bao la Carlos Tevez, hatua ambayo ilisababisha mabishano uwanjani.

Rais wa FIFA Sepp Blatter ambaye alipinga kutumika kwa teknolojia ya mstari wa golini alikuwepo katika uwanja wa Free State mjini Bloemfontein wakati England iliposhindwa 4-1 na Ujerumani, na kushuhudia refa kutoka Uruguay Jorge Larrionda na msaidizi wake Mauricio Espinosa wakishindwa kutambua kwamba mpira uliopigwa na Frank Lampard ulivuka mstari wa lango la Ujerumani.

Baada ya mechi hiyo kiungo huyo wa klabu ya Chelsea alitoa wito wa teknolojia ya mstari wa golini kuanza kutumika ili kuwasaidia marefa.

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron pia ni miongoni mwa wale waliosisitiza teknolojia hiyo ianze kutumika.

Tetesi za rais wa FIFA Sepp Blatter za kukataa teknolojia hiyo ni kwamba hatua ya kusimamisha mechi ili kuthibitisha ikiwa mpira umevuka mstari au la itavuruga mtiririko wa mchezo na engine hata kuinyima timu fursa ya kufunga bao.