Argentina kuhalalisha ndoa za jinsia moja

Wapenzi wa jinsia moja Argentina
Image caption Wapenzi wa jinsia moja Argentina

Bunge la Argentina limeunga mkono mswada wa sheria, inayolenga kuhalalisha ndoa za watu wa jinsia moja. Nchi hiyo sasa imekuwa ya kwanza kuhalalisha ndoa hizo katika Amerika ya kusini.

Mswada huo wa sheria ulikuwa ukipingwa vikali na Kanisa Katoliki na makundi mengine ya kidini.Bunge limeupitisha mswada huo kwa kura 33, huku upande uliopinga ukipata kura 27.

Wakati mjadala ukiendelea maandamano yalikuwa yakiendelea nje ya bunge. Baadhi ya waandamanaji walikuwa wakiupinga mswada huo, na wengine walikuwa wakiunga mkono.Rais wa nchi hiyo Cristina Fernandez, pia anaunga mkono.

Mkuu wa shirika la kutetea haki za watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja nchini Argentina Maria Rachid, ameelezea kuridhishwa na hatua ya wabunge kuunga mkono mswada huo. Amesema wametambua haki za watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.

Ndoa kadhaa za jinsia moja zimekuwa zikifanyika nchini Argentina,lakini baadhi zimekuwa zikitupiliwa mbali na mahakama ya ngazi ya juu na hivyo kusababisha mgogoro wa kisheria.

Ndoa za jinsia moja ni halali katika mji wa Buenos Aires na mikoa mingine lakini hakukua na sheria ya kuhalalisha ndoa hizo kote nchini.

Mji mkuu wa Argentina Buenos Aires, ni kati ya miji ambapo watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja wanakubalika zaidi, katika Amerika ya kusini.Ulikuwa mji wa kwanza kuhalalisha ndoa za jinsia moja.

Uhusiano wa jinsia moja ni halali nchini Uruguay, na katika baadhi ya majimbo ya Brazil, na nchini Mexico ndoa hizo ni halali.