Watibu wagonjwa wa ukimwi 'mapema'

Shirika la afya duniani WHO limesema katika muongozo wao mpya , vifo vinavyotokana na virusi vya HIV vinaweza kupunguzwa kwa asilimia 20 katika kipindi cha miaka mitano ijayo iwapo matibabu yatatolewa mapema.

Kuna watu zaidi ya milioni tano wanaopata matibabu ya kupambana na virusi hivyo mpaka mwisho wa mwaka 2009, zaidi ya milioni moja tangu 2008- ongezeko kubwa zaidi kutokea katika kipindi cha mwaka mmoja.

Muongozo huo utaongeza idadi ya watu wanaohitjai matibabu kufikia milioni 15 ifikapo mwaka 2015.

Lakini kuna wasiwasi wa ufadhili kwani nchi zimepunguza kiwango cha misaada inayotoa.

Image caption Dawa za kufubaza virusi vya ukimwi

Ikianza kutoa muongozo wake wa kwanza kwa kipindi cha miaka minne katika mkutano wa ukimwi 2010 mjini Vienna, WHO limesema linataka matibabu na mchanganyiko wa dawa kutolewa mwanzo kabisa kabla virusi havijafanikiwa kupunguza mfumo wa kupambana na maradhi wa mgonjwa.

Hii inamaanisha kubadilisha kiwango cha juu ambapo dawa hutakiwa kuanza kutumika kutoka seli 200 za CD4 kwa kila microlita ya damu mpaka 350, bila kujali dalili gani zimejitokeza.

Seli hizo ndizo huashiria afya halisi ya mfumo wa kupambana na maradhi ya mgonjwa.

Kuanza matibabu mapema kunaweza kuzuia kuenea kwa vijidudu kama vile kifua kikuu, ambao ni ugonjwa unaosbabisha vifo vingi kwa wale wenye virusi vya ukimwi.

Dr Gottfried Hirnschall mkurugenzi wa masuala ya HIV wa shirika la WHO, " Mbali na kuokoa maisha, matibabu ya mapema nayo yana faida ya kuzuia."

"Kwasababu matibabu hupunguza kiwango cha virusi mwilini, ina maana kutakuwa na uwezekano mdogo wa watu wenye virusi vya ukimwi kuwaambukiza wapenzi wao."

Kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa, kuongeza matibabu kwa watu zaidi kutaongeza gharama za mwaka 2010 kufikia hadi dola za kimarekani bilioni tisa.

Lakini wataalamu wanasisitiza gharama hizo za ziada zitafidia kwa kupunguza gharama za hospitali, kuongeza uzalishaji, kupungua kwa watoto yatima wanaotokana na kupoteza wazazi kutokana na ukimwi na kupungua kwa maambukizi mapya ya HIV.

Dr Bernhard Schwartlander wa UNAIDS alisema, " Uwekezaji tunaoweka sasa hautookoa tu mamilioni ya maisha ya watu lakini pia mamilioni ya dola kesho."