Afghanistan yataka kujidhibiti kiusalama

Kiongozi wa Afghanistan Hamid Karzai ametoa wito upya kwa nchi yake kudhibiti usalama wake ifikapo mwaka 2014 katika mkutano mkubwa wa kimataifa mjini Kabul.

Alikiri kuwa Afghanistan bado haijafanikiwa katika utawala bora.

Alikuwa akizungumza na wawakilishi kutoka mataifa 70 kwenye mkutano mkuu wa misaada uliowahi kutokea katika kipindi cha miongo mitatu.

Image caption Hamid Karzai wa Afghanistan akimkaribisha Bi Hollary Clinton wa Marekani

Marekani na washirika wake walitoa wito wakitaka Bw Karzai kutoa ahadi kuimarisha utawala bora.

Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, Rais wa Afghanistan aliahidi wazi kupambana na rushwa huku akiimarisha amani na maridhiano.

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron amesema kuondoa majeshi ya nchi hiyo ifikapo 2014 ni lengo linalowezekana.

Alisema mjini Washington kabla ya kufanya mazungumzo na Rais Barack Obama, " Tunatoa mafunzo kwa jeshi la Afghanistan kila mwezi na lengo hilo linaweza kutekelezwa."

Wachambuzi wanasema kwa kuwa wapiganaji bado wanadhibiti eneo kubwa Afghanistan, Bw Karzai ana nia thabit juu ya malengo ya usalama wa nchi yake.

Lakini Bw Ban, alisema haijawahi kutokea kukawa na mwelekeo mzito wa maisha ya usoni ya Afghanistan.