Afghanistan kusimamia usalama wake

Ramani ya Afghanistan

Mkutano mkuu wa wafadhili nchini Afghanistan umeidhinisha pendekezo la rais Hamid Karzai kuwa jeshi la nchi hiyo lianze kusimamia shughuli zote za usalama kufikia mwaka wa 2014.

Hata hivyo kuna hofu kuwa tangazo hilo la kujiondoa kwa majeshi ya kigeni huenda likalipa nguvu zaidi kundi la Taleban.

Makamanda wa kijeshi na wanasiasa waliokuwa wakikutana mjini Kabul wanadhani wamepiga hatua kuhusu mstakabal wa Afghanistan.

Wanamatumaini makubwa ya kuimarisha uwezo wa polisi na wanajeshi wa nchi hiyo. Kufikia sasa maafisa wa uslama wenyeji wanaongoza baadha ya operesheni nchini humo na wanahusika katika mipango ya uslama wakishirikiana na wanajeshi wa kigeni nchini Afghanistan.

Lakini tatizo ni kuwa wanajeshi na polisi vile vile mara kadhaa wanatoweka kazini, hawana elimu, baadhi ni walevi na idara hizo hazijawavutia watu wa kabila la Pashtun ambao ndio wengi nchini humo.

Lakini mashaka makubwa ni kuwa ufisadi umekithiri miongoni mwa polisi na kwa hivyo raia wa kawaida hawawamini. Inawezekana maarifa yao yameongezeka sana lakini ni robo tu ya idadi yote ya jeshi la Afghanistan ambalo lipo tayari kwenda vitani.

Kisa cha hivi karibuni ambapo mwanajeshi mmoja mzawa aliwashambulia wakufunzi wake pia kinaashiria hofu kuwa wapiganaji wa Taliban nao huenda wakapenyeza kwenye jeshi hilo na ikiwa hii ndio hali basi, juhudi za kuwa ajiri wanajeshi zitakuwa ngumu zaidi.

Ikiwa basi malengo ya kongamano hili yatafaulu, basi lazima Taliban washindwe nguvu, serikali za mtaa zenye uwezo mkubwa ziundwe na lazima rushwa ikomeshwe.

Haya yakitimia basi lengo hilo la wanajeshi wa Afghan kusimamia usalama wa nchi yao ifikiapo mwaka wa 2014 huenda likatimia lakini ni wazi hiki sio kibarua rahisi hata hivyo kwa sasa matumaini yapo.