ICC yashutumiwa kwa kuwalenga Waafrika

Image caption Rais Omar al-Bashir wa Sudan

Chad imeilaumu mahakama ya kimataifa inayokabili uhalifu (ICC) kwa kuwalenga viongozi wa Afrika pekee.

Kauli hiyo imetolewa wakati Rais wa Sudan Omar al Bashir akizuru nchi hiyo na kama njia ya kujitetea kwanini haikumkamata kiongozi huyo.

Rais huyo anatuhumiwa na mahakama ya kimataifa kwa mauaji ya kimbari na uhalifu wakati wa vita lakini yeye amekanusha madai hayo.

Chad ni nchi ya kwanza mwanachama wa ICC kumpokea Rais Bashir tangu ashitakiwe mnamo mwaka 2009.

Kesi zote tano zilizo mbele ya mahakama hiyo zinahusu Afrika ingawa makao ya mahakama hiyo yamedai kuwa ni jukumu la wanachama kutoa maelezo kama kuna kesi yoyote ya kupeleleza.

Umoja wa Afrika AU na Jumuia ya Mataifa ya kiarabu daima yamepinga uamuzi wa ICC wa kutoa hati za kuwakamata wahusika wa mgogoro wa huko Darfur.

Balozi wa Chad Ahmat Mahamat Bachir amesema kuwa nchi yake haikumkamata Bashir kwa kufuata msimamo wa AU, licha ya malalamiko kutoka kwa mashirika ya haki za binadamu.

Aliongezea kusema kuwa wapo viongozi wengine wanaostahili kulengwa kama Bw Bashir, bila kutaja ni viongozi gani wala wa nchi gani.

Bw Bashir anashtakiwa kwa kuwapa silaha mgambo wa kiarabu wanaotuhumiwa kwa kuwashambulia raia wenye asili ya kiafrika huko Darfur tangu makundi ya waasi yaanze kukabiliana na serikali mwaka 2003.

Kwa mujibu wa Umoja wa mataifa mgogoro wa Darfur umesababisha vifo vya watu 300,000 na wengine milioni mbili na laki saba kuhama kutoka kwao.

Serikali ya Sudan inakadiria watu 11,000 ndiyo waliouawa na kusema tatizo la eneo hilo limetiwa chumvi kwa sababu za kisiasa.

Bw Bashir yuko Chad kwa mkutano wa viongozi wa kikanda , jumuia ya Sahel na Sahara(Censad)

Nchi hizi jirani ziliwahi kulaumiana kwa kuanzisha vita baridi baina yao kupitia makundi ya waasi na Balozi wa Chad amesema kuwa jumuia ya kimataifa ilizitaka nchi hizo zijitahidi kuimarisha uhusiano mwema ili kuleta amani katika Darfur.