Chad haitamkamata Rais Bashir wa Sudan

Omar Al Bashir na Idriss Deby

Serikali ya Chad imesema kamwe haita mkamata Rais wa Sudan Omar Al Bashir ambaye yupo ziarani nchi humo, licha ya shinikizo kutoka kwa jamii ya kimataifa.

Chad imetakiwa imkamate Rais Bashir na kumkabidhi mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC kujibu mashtaka ya mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu.

Kesi dhidi ya Rais wa Sudan iliwasilishwa mwaka wa 2009 kufuatia machafuko yaliyokumba jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan.

Hii ndiyo mara ya kwanza Rais Bashir anazuru nchi iliotia saini mkataba unaotambua mahakama hiyo ya ICC.

Omar Al Bashir hangethubutu kufanya ziara nchini Chad mwaka mmoja uliopita. Kwa upande wake Rais Idriss Debby angepata afueni kumuona adui wake huyo akiwa gerezani kwa makosa ya kusababisha mauaji ya kimbari na uhalifu wa kibinadamu.

Kwa muda nchi mbili zimekuwa zikiunga mkono makundi ya waasi yaliyopinga serikali kutoka kila upande kitendo kilichotajwa kulipiza kisasi.

Mwaka 2008 kundi moja la Waasi likiungwa mkono na Chad lilikaribia sana mji mkuu wa Sudan Khartoum. Mapema mwaka huo kundi la waasi la Chad likiungwa mkono na utawala wa Khartoum nusura limpindue rais Idriss Deby ambapo lilizingira ikulu ya rais kabla ya kulemewa na wanajeshi kwenye makabiliano makali.Hali ilibadilika Januari mwaka huu viongozi hao wawili walipoamua kumaliza uhasama kati wao.

Rais Bashir alitaka jamii ya kimataifa kuheshimu serikali yake kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi. Naye Idriss Deby anayezingirwa na maadui nyumbani kwake alionelea kheri kufanya urafiki na jirani anayepakana naye badala ya kuendelea na uadui.

Huku Chad ikimkaribisha mgeni wake, baadhi ya makundi ya kutetea haki za binadamu yameghadhabika na kumuona rais Bashir kama anayekwepa kuwajibika kufuatia mauaji nchini mwake.

Kwa upande mwingine jamii ya kimataifa imeridhika na nchi mbili kuimarisha uhusiano kati yao. Hii ni kwa sababu urafiki huu unatoa nafasi ya kumaliza vita vinavyoendelea katika jimbo la Darfur ambalo huwa kwenye mpaka wa Chad na Sudan.

Baada ya Ziara hii, wengi wanasubiri kuona ikiwa rais Bashir ataamua kuhudhuria mkutano wa Muungano wa Afrika nchini Uganda unaofanyika juma hili. Uganda sawa na Chad zimesaini azimio linalotambua mahakama ya jinai ya ICC.

Mjini kampala adui mwingine wa zamani wa Bashir , rais Yoweri Museveni yuko tayari kumpokea kwa taadhima kuu.

Hata hivyo uhusiano kati ya nchi hizo mbili umekuwa siyo dhabiti sana na huenda kiongozi wa Sudan akaamua kutohatarisha uhuru wake hivyo kuelekea nyumbani punde akiondoka mjini Nd'jamena.