Uvamizi wa Iraq haukuwa wa busura

Sehemu moja ya Iraq wakati wa mashambulizi ya mwaka 2003
Image caption Sehemu moja ya Iraq wakati wa mashambulizi ya mwaka 2003

Mkaguzi mkuu wa silaha wa Umoja wa Mataifa, kabla ya mgogoro wa Iraq, Hans Blix, amesema Uingereza iliingia katika vita vya kuishambulia Iraq ambavyo havikuwa na sababu kisheria.

Bwana Blix alikuwa akizungumza na BBC mjini London, baada ya kutoa ushahidi wake mbele ya tume inayosikiliza sababu za kuivamia Iraq kijeshi.

Bwana Blix amehoji uamuzi wa aliyekuwa Rais wa Marekani George Bush na waziri wa zamani wa Uingereza Tony Blair kufanya pupa ya kuingia katika vita hivyo.

Hans Blix aliiambia tume ya wachunguzi mjini London kuwa, alishangaa ni kwa nini Marekani na Uingereza walidhana kufanyika kwa uchunguzi zaidi ulikuwa ni kupoteza muda. Anadai, wakati huo Iraq ilikuwa inaonyesha nia ya kushirikiana na uchunguzi wa shirika la umoja wa mataifa.

Blix alizishutumu nchi za Marekani na Uingereza kwa kuivamia Iraq bila ya kufanyika kwa uchuguzi zaidi.

Mkaguzi huyo wa zamani wa Umoja wa Mataifa, alisema kuwa hahoji iwapo rais George Bush wa Marekani na Tony Blair wa Uingereza walikuwa na nia njema walipoivamia Iraq, ila kile alichohoji ni uwamuzi wao wa kuchukua hatua hiyo.