Wyclef afikiria kugombea urais Haiti

Wyclef Jean
Image caption Wyclef Jean

Familia ya mwanamuziki aliyezaliwa Haiti imesema Wyclef Jean anafikiria kugombea urais nchini humo.

Lakini nyota huyo wa kundi la Fugees, ambaye aliteuliwa kama balozi wa nchi hiyo mwaka 2006, hajaamua bado kama agombee nafasi hiyo ya miaka mitano.

Haiti ilikumbwa na tetemeko kubwa la ardhi mwezi Januari iliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 250,000.

Taarifa kutoka familia yake ilisema Wyclef "anajali" sana maslahi ya kwao.

Taarifa hiyo ilitolewa baada ya kuwepo uvumi huko Haiti kuwa Wyclef anajiandaa kugombea nafasi hiyo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba.

Wagombea wana nafasi ya kujiandikisha mpaka ifikapo Agosti 7.

Ilisema: " Namna Wyclef anavyojali maslahi ya kwao hauna mipaka kabisa na ataendelea kuisaidia nchi yake bila kujali kama yeye ni sehemu ya serikali.

"Kwa wakati huu, Wyclef Jean hajatangaza nia yake ya kugombea Urais Haiti. Iwapo, na wakati, uamuzi utakapochukuliwa, vyombo vya habari vitapewa taarifa haraka iwezekanavyo."

Rais aliye madarakani kwa sasa Rene Preval anazuiwa na katiba kugombea nafasi hiyo kwa mara nyingine.

Wyclef, anayeishi New York, ni mwanzilishi wa wakfu wa kusaidia binadamu ya Yele Haiti, na amechangia kwa kiasi kikubwa katika kutoa misaada tangu kutokea kwa tetemeko hilo la ardhi.

Mwanamuziki huyo na mzalishaji wa muziki, anayejulikana zaidi sasa kwa kushirikiana na mwanamuziki nyota wa miondoko ya Pop kutoka Colombia Shakira, anajulikana sana Haiti ambapo nusu ya watu wote nchini humo wana umri wa miaka 21.