Jeshi la Uingereza lafanikiwa Afghanistan

Jeshi la Uingereza
Image caption Jeshi la Uingereza

Majeshi ya Uingereza yanaarifiwa kupata mafanikio katika operesheni mpya ya kuwafurusha wapiganaji wa kundi la Taleban kutoka ngome yao kubwa kusini mwa Afghanistan.

Operesheni ya Tor Shezada ilianza mapema siku ya Ijumaa katika jimbo la Helmand, huku wanajeshi wakidondoshwa na ndege za helicopter karibu na mji wa Saidabad.

Waasi wanadhaniwa kutumia eneo hilo kutengeneza mabomu na kutekeleza mashambulizi.

Major Simon Ridgway, wa jeshi la Uingereza, alisema wanajeshi wao "waliteka" maeneo ambayo waliyalenga hapo awali.

Mamia ya wanajeshi wa Uingereza na Afghanistan wanashiriki operesheni hiyo.

Wanajeshi hao wanajaribu kuwaondoa wanamgambo wa Taliban kutoka ngome yao kuu wilayani Nad Ali.

Eneo la Saidabad ni mojawapo ya maeneo ambayo wanajeshi wa Uingereza walishindwa kuwaondoa wanamgambo katika operesheni ya Moshtarak mapema mwaka huu.

Zaidi ya wanamgambo 180 wanadhaniwa kutumia mji huo kama ngome kuu.

Akitathmini mafanikio ya majeshi katika operesheni hiyo, Maj Ridgway aliambia BBC "tuliteka maeneo ambayo awali tulitaka kurejesha usalama na sasa tunaendelea kufahamu vema mahali ambapo tulipo".

Afisa huyo aliongeza kuwa wanapata mafanikio katika operesheni ya kuwafurusha waasi kutoka Saidabad.

Maj Ridgway alisema kulikuwa na mapambano madogo ya kufyatuliana risasi lakini hilo halikuwapa wasiwasi.