RBS yakanusha kuzungumza na Huang

Benki ya Royal Bank of Scotland inayoidai club ya Liverpool, imekanusha habari kuwa inafanya mazungumzo na mfanyabiashara wa Uchina Kenny Huang kununua deni la pauni milioni 237 kama hatua ya kwanza katika kuimiliki.

Magazeti na vyombo vingine vya habari hapa Uingereza vimetoa maelezo kwamba ana uhusiano wa karibu na mchezo wa baseball na vilevile mchezo wa kikapu nchini Marekani amewasiliana na Benki hiyo kwa ajili ya kununua deni hilo kama hatua ya kwanza katika kuimiliki Liverpool.

Vyombo vya habari vimesema kuwa Huang, raia wa Marekani mzaliwa wa Guangdong amefanya mazungumzo na Benki hiyo.

Msemaji wa benki ya RBS ameliambia shirika la habari Reuters kuwa hakuna mtu yeyote aliyewasiliana nao kuhusu Liverpool.

Huang ambaye anamiliki kampuni ya vifaa vya michezo mjini Hongkong QSL Sports group hajatoa tamko lolote kuhusu mpango huo ila ameajiri kampuni moja ya Uingereza kumuwakilisha kwa shughuli zote kuhusu kuinunua club hiyo.

Ikumbukwe kuwa wamiliki wa Liverpool waliamuru Benki yao Barclays capital kutafuta mnunuzi mapema mwezi April mwaka huu na kumteua mwenyekiti wa British Airways, Martin Broughton kusimamia shughuli ya kuiuza.

Image caption Kenny Huang

Hata hivyo Barclays imekataa kutoa kauli yoyote.

Huang hajasema lolote kuhusiana na mpango huu lakini duru iliyotoa habari hizi imesisitiza kuwa Huang ameitikia hatua ya wamiliki wa club hiyo Tom Hicks na George Gillet ya kutangaza kutaka wanunuzi wajitokeze mapema mwezi April.

Ingawa Huang ambaye ni mwenyekiti wa kampuni ya QSL Sports yenye makao yake Hong Kong ameajiri kampuni moja ya Uingereza kumwakilisha katika shughuli ya kuinunua klabu yenye sifa ya kuwa bingwa mara tano wa Ulaya.

Huang anamiliki hisa ndogo katika klabu ya mchezo wa kikapu nchini Marekani Cleveland Cavaliers.

Kuna habari nyingine kuhusu mfanyabiashara wa Syria ambaye hapo zamani aliwahi kucheza mpira wa kulipwa kimataifa Yahya Kirdi naye amehusishwa na tetesi za kuinunua klabu ya Liverpool.