Mchina kuinunua Liverpool?

Image caption Martin Broughton

BBC imefahamu kwamba mfanyabiashara wa Kichina Kenny Huang ni mmoja kati ya wanunuzi kadhaa waliowasilisha maombi yao kwa mwenyekiti wa Liverpool Martin Broughton kwa kutaka kuinunua klabu hiyo.

Huang ambaye ni mkuu wa kampuni ya uwekezaji mjini Hong Kong QSL Ltd anaikadiria klabu hiyo kuwa na thamani ya pauni za Uingereza milioni 325.

Imefahamika sasa kuna watu wasiopungua sita waliojitosa kuinunua.

Mwenyekiti Broughton pamoja na kitengo cha uwekezaji cha benki ya Barclays, wanaosimamia biashara ya Liverpool watachagua mshindi kabla ya mwisho wa juma lijalo.

Huang amefanya mazungumzo na wawakilishi wa Benki ya RBS (Royal Bank of Scotland) kwa nia ya kuimiliki kikamilifu Liverpool ambayo ilitangazwa kuuzwa tangu mwezi Aprili mwaka huu.

Liverpool inadaiwa na RBS takriban pauni milioni 237 zilizotumiwa na wamiliki wa klabu hiyo Tom Hicks na George Gillett.

Ingawa RBS imekana kuzungumza moja kwa moja na Huang, lakini inaeleweka kuwa amejenga ombi la kuridhisha.

Huang amejitolea kulipa deni lote linalokwamisha maendeleo ya klabu akitaka pia kuondoa mashaka yote na kumpa Kocha Roy Hodgson fedha za kusajili wachezaji kabla ya wimbi la usajili kufungwa.

Hata hivyo, tajiri huyo anataka mpango mzima umalizike katika kipindi cha majuma mawili ili Hodgson apate muda wa kusajili wachezaji kabla ya msimu mpya na vilevile yuko tayari kutoa fedha zaidi za ujenzi wa uwanja mpya.

Huang ni mtu maarufu katika sekta ya michezo huko Uchina akiwa na ushawishi mkubwa katika mchezo wa kikapu na baseball.

Kampuni yake ya QSL Ltd ni mshirika wa timu ya mchezo wa kikapu nchini Marekani ya Cleveland Cavaliers akiwa mshirika na kundi la baseball la New York Yankees.

Mnamo mwaka 1988, alikuwa mwanafunzi Mchina wa kwanza kutoka Uchina kufanya kazi katika soko la hisa lijulikanalo kama New York Stock Exchange.

Imearifikwa kuwa aliwahi kukataa kuinunua Liverpool mwaka 2008 kwa kuhisi kiwango kilichotakiwa cha pauni milioni 650 kilikuwa juu sana.

Hicks na Gillett waliinunua mwezi Febuari 2007 kwa pauni milioni 218.9 ikiwa na deni la pauni milioni 44.8

Tangu hapo Wamarekani hao wamekuwa na wakati mgumu, ambapo mashabiki wameonyesha hasira zao kwa kiwango cha madeni kilichofikiwa tangu wamiliki hao wainunue klabu ya Liverpool.