Israil na Lebanon zasitisha mapigano

Wanajeshi mpakani mwa Israil na Lebanon
Image caption Wanajeshi mpakani mwa Israil na Lebanon

Hali ya utulivu imerejea mpakani mwa Israil na Lebanon, baada ya mapigano makali kuzuka hapo jana kati ya majeshi ya pande hizo mbili.

Wanajeshi wawili wa Lebanon, na mwandishi mmoja wa habari waliuawa katika mapigano hayo. Mwanajeshi mmoja wa Israil, pia alipigwa risasi na kuuawa.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, ametoa wito kwa pande hizo mbili kuzingatia utulivu.

Majeshi ya Umoja wa Matifa Kusini mwa Lebanon, wameimarisha doria na kutangaza matokeo ya uchunguzi wao, kuhusu chanzo cha mzozo huo.

Wamesema wanajeshi wa Israil, hawakuwa wamevuka eneo la mpaka.

Hatahivyo, Lebanon ambayo inaishtumu Israil kwa kukiuka kanuni za Umoja wa Mataifa, imepinga matokeo hayo ya uchunguzi.

Na huku wanajeshi wa pande hizo mbili wakiwekwa katika hali ya tahadhari, juhudi za kidiplomasia zikiongozwa na Umoja wa Mataifa zinaendelea ili kuepusha mapigano zaidi .