Kura ya maoni Kenya yafanyika kwa amani

Milolongo ya wapiga kura
Image caption Milolongo ya wapiga kura

Shughuli ya kupiga kura ya maoni kupinga au kuunga mkono katiba mpya inayopendekezwa nchini Kenya imemalizika.

Shughuli hiyo imefanyika kwa njia ya amani, na watu walijitokeza kwa wingi kushiriki.

Kulikuwa na milolongo mirefu ya watu katika vituo vya kupiga kura, na vituo vingi viliendesha shughuli zake bila matatizo.

Vituo vya kupigia kura vilifungwa saa 11 kamili, na kuruhusu tu wananchi waliokuwa wamefika vituoni wakati huo kupiga kura.

Katika baadhi ya vituo kura zimeanza kuhesabiwa.

Image caption Wananchi wakipiga kura mapema asubuhi

Katiba hiyo mpya inayopendekezwa, inatazamiwa kubadilisha mwelekeo wa siasa za Kenya, na kuwaepusha raia wa nchi hiyo kujipata katika ghasia kama zile zilizotokea baada ya uchaguzi mkuu wa Desemba mwaka 2007.

Zaidi ya watu 1,000 walikufa kufuatia matokeo ya uchaguzi yaliyokumbwa na utata. Wanaounga mkono katiba hiyo wanasema itayapunguza madaraka ya rais, na vile vile kutatua masuala muhimu kuhusiana na ardhi.

Upande unaounga mkono katiba hiyo, unaongozwa na Rais Mwai Kibaki na waziri mkuu Raila Odinga ambaye amesema ana imani kuwa upande wake utajipatia ushindi.

Wanaoipinga katiba hiyo akiwemo Rais mstaafu Daniel Arap Moi na wanasema iwapo itapitishwa itayafanya mambo kuwa mabaya zaidi nchini humo.

Naye Waziri wa Elimu ya Juu, William Ruto, ambaye aliongoza kampeni za kupinga katiba hiyo inayopendekezwa amesema mrengo wake unakabiliwa na jukumu muhimu ikiwa utashinda ama kushindwa.

Matokeo ya mapema yanatarajiwa kuanza kutangazwa kuanzia saa nne usiku (Kenya) na matokeo rasmi kutangazwa hapo siku ya Ijumaa.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii