Ligi kuu ya England kutokota

Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya msimu mpya wa Ligi kuu ya England kuanza, bingwa mtetezi Chelsea pamoja na klabu inayotishia kushinda ligi kila msimu Manchester United vinajiandaa kukabiliana na kitisho cha klabu ya Manchester City.

Man City imetumia pesa nyingi kusajili wachezaji wazuri kutoka kila pembe ili kuimarisha kikosi chake.

Image caption Robert Mancini

Wakati meneja wa Chelsea Carlo Anceloti na Sir Alex Ferguson wakiridhika kwa kuongezea wachezaji wachache, Roberto Mancini amekuwa katika shughuli ya kusajili wachezaji mfano wa mtu aliyeshinda kamari.

Hadi sasa Mancini ametumia pauni za Uingereza milioni 80 kwa wachezaji wanne tu kwa kutegemea utajiri wa wamiliki wapya wa klabu hiyo yenye makao yake huko Abu Dhabi wanaohisi kwamba pesa itawapa ufanisi wanaohitaji wa kushinda ligi hiyo.

Usajili wa Yaya Toure kutoka Barcelona, David Silva kutoka klabu ya Valencia, Alexander Kolarov wa Lazio na beki wa Hamburg ya Ujerumani Jerome Boateng ni taarifa tosha ya nia ya kutaka mafanikio.

Na kama hayo hayatoshi, Mancini bado anatazamia kumsajili Mario Balotelli kutoka Milan kwa kitita cha pauni milioni 25 pamoja na kutoa nyingine 25 kwa kumng'oa James Milner kutoka Aston Villa.

Mfano wa Man City huenda usiwavutie wapenzi wa mfumo wa kujenga timu kuanzia chekechea, lakini mfano wa Chelsea na Blackburn zilipoibuka kupata ufanisi kwa kutumia pesa unatosha kuwaridhisha mashabiki wa Man City ambao tangu mwaka 1968 hawajaona Kombe la ligi kuu.

Meneja wa Chelsea, Ancelotti ameonyesha wasiwasi na kukiri kuwa kweli klabu ya mwananchi mwenzake Mancini inatisha.

Ancelotti aliongezea kusema ni vigumu kujenga timu katika msimu mmoja, lakini Roberto Mancini ana uzoefu wa kufanya hivyo.

Umwagaji wa fedha unatukumbusha enzi za Roman Abramovich alipotumia pesa nyingi kubadili majaaliwa ya Chelsea na kuifanya klabu hiyo kuwa bingwa.

Image caption Carlo Ancelloti

Hiyo ni enzi iliyopitwa na wakati kwa Ancelotti na kwa sasa mtaalamu huyo imebidi atumie uzi wa kutosha nguo iliopo kwa kusajili idadi ndogo ya wachezaji kwenye kambi ya Chelsea.

Ingawa amewapoteza Michael Ballack, Joe Cole na Juliano Belletti, kocha huyo amemsajili mcheza kiungo Yossi Benayoun kutoka Liverpool.

United kwa upande wake imezongwa na madeni makubwa na hivyo kupunguza joto la usajili katika kipindi hiki.

Ferguson ana imani na mshambuliaji Javier Hernandez kutoka Mexico mwenye umri wa miaka 22, mshambuliaji wa Italia Federico Macheda mwenye umri wa miaka 18 na beki Chris Smalling, 20, kutoka Fulham akisema hawa wataziba pengo tutakaposuasua.

Na miaka mitano bila kombe lolote, meneja wa Arsenal, Arsene Wenger ana matarajio makubwa ingawa huenda mipango yake ikachafuliwa na hamu ya nahodha wake Cesc Fabregas kujiunga na klabu ya Barcelona.

Nina imani ya kufanya vyema msimu huu, alisema Wenger. Msimu uliopita tulimaliza wa tatu nadhani tunaweza kupiga hatua zaidi ya hapo.

Mwishoni mwa msimu uliopita Tottenham ilionyesha kuwa si klabu ndogo tena kwa kumaliza ya nne na huenda safari hii inalenga mbali zaidi kujishindia ligi.

Mabadiliko yaliyofanywa huko Anfield kwa kumleta kocha aliyefanikiwa na klabu ya Fulham huenda kukabadili mambo na kupandisha klabu iliyoshindwa kushikilia nafasi yake kati ya nne bora za England ikimaliza katika nafasi ya saba.

Hata hivyo Roy Hodgson ana kibarua cha kufasiri mafanikio yake huko Fulham na kuyaonyesha kwa mashabiki wa Liverpool.