Spurs wachemsha

Pavlyuchenko
Image caption Pavlyuchenko

Katika michuano ya Ligi ya mabingwa iliyofanyika usiku wa Jumanne, wawakilishi wa England Tottenham hotspurs walitatizika katika jaribio lao la kwanza bila kushiriki michuano ya Ulaya tangu klabu hiyo ishiriki nusu fainali ya Kombe la Ulaya la msimu wa mwaka 1960/61.

Klabu hiyo iliyoonyesha mchezo wa kusisimua katika Ligi kuu ya England dhidi ya Manchester City siku ya Jumamosi iliyopita, ilibadilika mbele ya klabu ambayo wengi walidhani ni kibonde, Young Boys kutoka Uswizi.

Kabla ya pambano hilo Spurs ilipewa kila fursa kuiondoa klabu hiyo ya Young Boys kwa urahisi lakini Young Boys walikuwa na fikra tofauti wakitumia uwanja bandia kwa ustadi wa juu na kwa kipindi cha nusu saa Kocha Harry Redknapp hakuamini kilichowafika vijana wake.

Katika hali ya kuchanganyikiwa Senad Lulic akaliona lango la Spurs.

Hii ni baada ya shuti ya Thierry Doubai kumgonga Ammar Jemal, aliyeonekana kuwa kaotea lakini ukamwangukia Lulic aliyekuwa umbali wa yadi nane hivi na kuzitikisa nyavu za Spurs.

Spurs hata hivyo walipata fursa ya kurudisha bao hilo lakini kipa Marco Wolfli akapangua njama hiyo.

Kocha Redknap aliyewaacha nje baadhi ya nyota wa timu yake alitumia mfumo wa 4-4-2, na kabla ya kujituliza wakabamizwa kwa bao la pili kufuatia pasi nzuri kutoka kwa kiungo Costanzo iliyomfika Hochstrasser bila upinzani wa mabeki akautuliza kimyani mpira kuhesabu la pili kwa Young Boys.

Image caption Robbie Keane

Hapa ndipo Redknapp alipoamua kumuondoa beki Assou Ekotto na badala yake kumleta kiungo Huddlestone mnamo dakika ya 35.

Wakati huu wachezaji wa Spurs walikuwa wameanza kuuzoea uwanja bandia na Bassong akipokea mpira wa kona uliochongwa na Gareth Bale akauelekeza kimyani kuhesabu la kwanza kwa Spurs.

Muda mfupi baada ya bao hilo Pavlyuchenko akakosa bahati ya wazi kuutokomeza kimyani mpira uliotoka kwa Bale.

Uwezekano wa kurudisha mabao yao uliwaamsha Young Boys waliotiririka na mpira na kuongezea la tatu huku Spurs wakihangaika kuokoa jahazi.

Baada ya kosa kosa kadhaa, juhudi za Pavlyuchenko zilizaa matunda alipopokea pasi kutoka kwa Robbie Keane na kutoa kombora lilioipa Spurs matumaini ya kubadili nyota yao katika mechi ya marudiano kwenye uwanja wa Spurs wa White Hart lane, jijini London.

Kwingine katika michuano hiyo hiyo Dynamo Kiev ilitoka sare 1-1 na Ajax, Rosenborg ikaichapa FC Copenhagen 2-1, Sparta Prague ikanyukwa na MSK Zilina 2-0, Zenit st Petersburg ikaishinda Auxerre 1-0