Jaji afuta mashtaka dhidi ya maharamia wa Kisomali

Askari wa kimataifa akimpekua mtuhumiwa wa uharamia
Image caption Askari wa kimataifa akimpekua mtuhumiwa wa uharamia

Jaji mmoja nchini Marekani ametupilia mbali baadhi ya mashtaka dhidi ya washukiwa sita wa uharamia kutoka Somalia.

Washtakiwa hao wanatuhumiwa kuishambulia meli ya wanamaji wa Marekani katika pwani ya Afrika Mashariki.

Jaji huyo amesema mashtaka hayo ya wizi, kuingia katika chombo hicho bila ruhusa na kuchukua udhibiti wake sio makosa ya uharamia.

Hata hivyo washukiwa hao baado wanakabiliwa na mashtaka mengine saba katika mahakama moja katika jimbo la Virginia.

Washukiwa hao, waliokamatwa na jeshi la wanamaji la Marekani mwezi Machi mwaka huu, wanakabiliwa na mashitaka ya uharamia, kushambulia chombo cha baharini, na matumizi ya silaha.

Idadi kubwa ya meli za kivita za kimataifa zinapambana na uharamia kwenye maji ya Somalia, eneo ambalo sheria hukiukwa.

Somalia imekuwa bila ya serikali thabiti tangu mwaka 1991, hali ambayo imesababisha uvunjaji wa sheria na kuwapa mwanya maharamia kuendesha shughuli zao katika pwani ya nchi hiyo bila kuchukuliwa hatua zozote.