Muambukiza UKIMWI aepuka jela Ujerumani

Nadja Benaissa
Image caption Nadja Benaissa

Mwanamziki wa miondoko ya Pop wa Ujerumani anayeishi na virusi vya Ukimwi anayetuhumiwa kumwambukiza mpenzi wake virusi vya ugonjwa huo amepewa kifungo cha nje cha miaka miwili.

Nadja Benaissa, mwenye umri wa miaka 28, alikiri kufanya mapenzi bila kujikinga na kuficha hali yake ya kiafya, lakini amekana kumwambukiza mwenzake kwa makusudi.

Mwimbaji huyo wa kundi la No Angels alikutwa na kosa la kusababisha madhara kwa mtu mmoja, na makosa mawili ya kujaribu kumdhuru mtu.

Katika kesi hiyo alisema, " anaomba radhi kwa moyo wake wote."

'Uwoga'

Bi Benaissa alifanya mapenzi na watu watatu bila ya kuwaambia kuwa ameathirika. Mmoja wao alithibitishwa kuambukizwa virusi hivyo.

Bi Benaissa aliiambia mahakama kwamba hakumwambia mtu yeyote kuhusu maradhi yake kwasababu alikuwa na wasiwasi wa matokeo hasa ya kazi yake, ambapo alisema lilikuwa ni "suala la uwoga."

Alidai aliambiwa na madaktari kuwa hatari ya kumwambukiza mtu virusi ni "sawa na kuwa haiwezekani."

Bi Benaissa alikamatwa mjini Frankfurt mwaka jana, muda mfupi kabla ya kushiriki kwenye tamasha, na kuwekwa kizuizini kwa siku 10.

Kundi la No Angels liliundwa mwaka 2000 katika kipindi cha kimataifa cha televisheni cha Popstars, kabla ya kurekodi mfululizo wa nyimbo maarufu na kuibuka kundi lenye mafanikio makubwa Ujerumani.

Mwaka 2007 waliibuka upya na kushindana katika mashindano ya Eurovision mwaka 2008, na kuchukua nafasi ya 23.