Wafanyakazi zaidi wagoma Afrika Kusini

Maafisa wa polisi wakiwatawanya waandamanji Afrika Kusini
Image caption Maafisa wa polisi wakiwatawanya waandamanji Afrika Kusini

Wafanyakazi wa umma nchini Afrika Kusini ambao mgomo wao kuhusu nyongesa ya mishahara, unaingia wiki yake ya pili, wametangaza kuwa watafanya maandamano katika maeneo yote nchini humo.

Serikali ya nchi hiyo, imekataa kuidhinisha nyongesa ya mishahara ya asilimia nane nukta sita na badala yake kuhaidi kutoa asilimia saba pekee.

Wafanyikazi karibu 10,000 wa sekta ya umma wamekuwa wakiendelea na maandamano mjini Johannesburg, kama ishara ya kuungana na wenzao waliogoma, ikiwa ni siku ya nane leo.

Maandamano hayo yaliendelea kwa hali ya utulivu, licha ya kelele, na shughuli nyingi kusitishwa mjini.

Maafisa wa polisi walikuwa wengi pia mjini, na ni amri ya dakika za mwishomwisho iliyotolewa na mahakama iliyowazuia wasijiunge na mgomo.

Migomo kama hiyo ya wafanyikazi wa umma imefanyika sehemu mbalimbali za nchi.

Chama cha wafanyikazi, COSATU, kimeelezea kwamba mgomo huo unachangia katika kuleta mvutano kati yake na chama kinachoiongoza serikali ya nchi hiyo, ANC.