Rudisha avunja rekodi yake ya mita 800

David Rudisha amevunja rekodi ya mbio za mita 800 kwa mara ya pili katika kipindi cha siku nane mjini Rieti, Italia.

Rudisha kutoka Kenya mwenye umri wa miaka 21 alikimbia kwa muda wa dakika moja sekunde 41.01.

Muda mzuri kabla ya hapo ulikuwa wa dakika moja sekunde 41.11 uliowekwa na mwanariadha mzaliwa wa Kenya aliyekuwa akikimbilia Denmark Wilson Kipketer mwaka 1997.

Katika mashindano hayo ya Italia, mwanariadha kutoka Jamaica Nesta Carter aliweza kukimbia muda sawa uliowekwa na Tyson Gay kwa mwaka huu wa 2010 wa sekunde 9.78 katika mbio za mita 100.

Rudisha alikuwa na matumaini makubwa angevunja rekodi na alikuwa anaamini angeiporomosha rekodi ya dunia.

Alisema: "Nilielewa nilikuwa katika hali nzuri. Hali ilikuwa ni ya kupendeza. Nilitarajia ningevunja rekodi kwa muda wa wiki moja".

Rudisha ni bingwa wa Afrika katika mbio hizo zamita 800 lakini aliweza kufika hatua ya nusu fainali katika mashindano ya ubingwa w dunia mwaka 2009.