Malipo ya wafanyakazi A Kusini yaongezwa

Serikali ya Afrika Kusini imeongeza ahadi ya kiwango cha mshahara kwa zaidi ya milioni kwa wafanyakazi wa umma waliogoma.

Rais Jacob Zuma alitoa wito wa kuanza upya mazungumzo baada ya mgomo huo wa wiki mbili kusababisha shule na hospitali nyingi kusimamisha shughuli zake.

Image caption Mgomo Afrika Kusini

Baada ya kuwa na mjadala mzito usiku kucha, wawakilishi wa serikali wameongeza malipo hayo kwa asilimia 7.5.

Vyama vya wafanyakazi vimekuwa vikitaka ongezeko la asilimia 8.6 na wanatarajiwa kupiga kura siku ya Jumanne usiku kuamua wakubali ongezeko hilo au la.

'Hatua ya ushindi?'

Zwelenzima Vavi, katibu mkuu wa shirikisho kuu la vyama vya wafanyakazi, Cosatu, aliiambia BBC kuwa walipambana vilivyo katika mazungumzo hayo ili kuishinikiza serikali iongeze mshahara kwa asilimia nane.

Alisema ni uamuzi wa wanachama iwapo watakubaliana na ongezeko hilo.

Image caption Mgomo Afrika Kusini

" Jana usiku tulipambana vilivyo na mpaka kufika asubuhi haikuwezekana.. Nahisi itabidi mgomo kama huu wa takriban wiki moja au mbili ufanyike ndio serikali itakubali matakwa yao."

"Swali ambalo wanachama wetu wanatakiwa kujibu kwa sasa ni: je ni muhimu-ukizingatia masuala yote hayo- au ni hatua ya ushindi katika kipindi tulichofikia sasa?"

Mgomo huu umeathiri zaidi mahospitali, ambapo wauguzi wa kijeshi na watu waliojitolea wakiendelea kuwahudumia wagonjwa.

Mwandishi wa BBC mjini Johannesburg Karen Allen alisema, kabla ya mazungumzo ya hivi karibuni kufanyika, Cosatu ilitishia kufanya mgomo wa siku moja Alhamis iwapo ongezeko hilo la malipo kwa asilimia 8.6 halitofikiwa.

Takriban wafanyakazi wa umma milioni moja tayari wamegoma.

Mwandishi wetu alisema haiko wazi iwapo watatekeleza tishio lao hilo.

Alisema, hatua ya Bw Zuma kurejesha upya mazungumzo limechochewa zaidi na siasa kuliko hata uchumi.

Bw Zuma amekuwa akikosolewa na wafanyakazi hao waliogoma kuwa alikuwa katika ziara ya kibiashara huko China- huku wauguzi, walimu na wafanyakazi wengine wa umma wakiwa mitaani wakitaka ongezeko la mishahara.

Karen Allen alisema kuwa inambidi Rais huyo arejeshe mahusiano mazuri na vyama hivyo, ambapo ni ngao yake muhimu, kabla ya kuwepo mkutano wa sera wa chama tawala, the African National Congress, katika kipindi cha wiki tatu.