Asamoah Gyan ajiunga na Sunderland

Asamoah Gyan
Image caption Asamoah Gyan

Klabu ya Sunderland amevunja rekodi ya usajili baada ya kufanikiwa kumsajili mshambuliaji Asamoah Gyan kutoka klabu ya Rennes kwa dau la paundi milioni 13, kwa mujibu wa Sunderland.

Asamoah mwenye umri wa miaka 24, aliyepachika mabao matatu kwa timu yake ya taifa ya Ghana katika mashindano ya fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini, amesaini mkataba wa miaka minne.

Aliwasili katika klabu hiyo siku iliyotangazwa mshambuliaji wa Sunderland Fraizer Campbell hatacheza kwa takriban miezi sita baada ya kuumia goti.

Meneja wa Sunderland Steve Bruce amefurahishwa baada ya kufanikiwa kukamilisha mkataba wa kumsajili Asamoah Gyan.

Alisema alijaribu kumsajili msimu uliopita lakini ilishindikana.

Gyan mwenyewe amesema amefarijika kujiunga na Sunderland na kuwapongeza mashabiki wa klabu hiyo kwa kutokata tamaa.

Amesema amekuwa akifuatilia soka ya Uingereza na anafahamu Sunderland ina mashabiki wenye msimamo.

Mshambuliaji huyo alianza kusakata soka na klabu ya Liberty ya Ghana kabla hajaelekea Italia alikojiunga na klabu ya Udinese mwaka 2003.

Mwaka 2008 klabu ya Ufaransa ya Rennes iliilipa Udinese paundi milioni 6.6 kwa ajili ya kumnunua mshambuliaji huyo ambaye aliifungia klabu hiyo mabao 14 katika mechi 47 alizocheza.