Marekani yalaani mauaji ya Wayahudi

Katika mkesha wa mazungumzo ya ana kwa ana baina ya Wapalsetina na Israeli, Marekani imeziomba pande hizo mbili zisiruhusu mauaji ya Wayahudi wanne karibu na Hebron yapangue juhudi zao za kuleta amani.

Raia wanne wa Israeli waliuawa kwa risasi katika ukanda wa magharibi siku ya Jumanne.

Tawi la kijeshi la vuguvugu la kundi la Kipalestina la Hamas lilidai kuhusika na mauaji hayo na kujisifu kama la kishujaa.

Image caption Waisrael wanne wapigwa risasi na kufa katika ukanda wa magharibi wa mto Jordan

Viongozi wa Palestina na Israeli wanakutana Alhamisi kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka miwili.

Wakati wa kuandaa mazungumzo hayo mjini Washington, Ikulu ya Marekani imelaani vikali mauaji hayo na kutaka pande hizo mbili husika zijitahidi kufikia amani ya dhati na ya kudumu katika Mashariki ya kati.

Kabla ya kukutana na waziri mkuu Benjamin Netanyahu wa Israeli siku ya Jumanne, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Bi Hillary Clinton ameihakikishia Israel usalama.

Bi. Clinton alisema, "Tunajitolea kuwa daima tutafanya kila tuwezalo kulinda na kutetea taifa la Israeli pamoja na kulinda usalama wa raia wake,"

Msemaji wa Bw Netanyahu, Nir Hefetz, alisema waziri mkuu aliamuru vikosi vya usalama vichukue hatua bila kujali vikwazo vya kidiplomasia ili kuwakamata wauaji.

Bw Hefetz aliongezea kusema "Ugaidi kamwe hautoamua mipaka ya Israeli wala majaliwa ya makaazi ya walowezi Wayahudi.

Waziri mkuu wa Palestina Salam Fayyad naye amelaani mauaji hayo akisema yanakwenda kinyume na mahitaji ya Wapalestina.

''Shughuli''

Image caption Bi Hillary Clinton

Viongozi wa Palestina na Israeli wanakutana na Bi Clinton Alhamisi na hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa Rais wa Palestina Mahmood Abbas na Bw Netanyahu kuwa katika chumba kimoja kwa zaidi ya mwaka mmoja. Katika kuandaa mazungumzo hayo, Rais Barack Obama atakutana na Bw Netanyahu na Bw Abbas.

Vile vile anatarajiwa kukutana na Mfalme Abdullah wa Jordan na Rais wa Misri Hosni Mubarak.