Talaka ya Cheryl na Cole yaruhusiwa

Talaka ya Cheryl na Ashley Cole imeruhusiwa na mahakama kuu baada ya ndoa yao ya miaka minne kuvunjika.

Image caption Mahakama imekubali waachane

Jaji Christopher Simmonds ndiye aliyekuwa kizimbani na kutoa ruhusa ya kuvunja ndoa hiyo kisheria kutokana na Ashley Cole mwenyewe kukiri kuwa na tabia zisizostahiki.

Wapendanao hao walitengana mwezi Febuari baada ya madai kuchapishwa kwenye magazeti kuhusu mchezaji wa Timu ya Taifa ya England na Chelsea kwa tabia za uzinzi.

Walikutana mwaka 2004 walipokuwa wakiishi katika jengo moja mjini London.

Punde baada ya hapo walikubaliana wafunge ndoa Cole alipomuomba uchumba wakiwa Dubai.

Mwaka 2006 walifunga ndoa kwenye sherehe ya kifahari huko Hertfordshire.

Mwaka 2008, ndoa ikatetereshwa na madai ya magazeti kuhusu tabia ya Ashley Cole ya kutokatoka ovyo na wanawake.

Kufuatia madai hayo, ndoa yao ikawa ikifuatiliwa kwa karibu na magazeti, na mara kwa mara Cheryl alipigwa picha bila pete yake ya ndoa.

Mahakamani leo walipewa kinachojulikana kama 'decree nisi' hatua ya kwanza ya mchakato wa kufikia talaka ikimaanisha umesalia muda wa wiki chache kukamilisha talaka kamili.