Klitschko amuonya Haye asipayuke ovyo

Wladimir Klitschko
Image caption Wladimir Klitschko

Wladimir Klitschko amemwambia David Haye aache kuzungumza "upuuzi" na badala yake wakutane ulingoni kwa pambano la kuunganisha mataji matatu ya ubingwa wa uzito wa juu duniani.

Klitschko amefanikiwa kutetea mataji yake ya WBO na IBF baada ya kumdondosha katika raundi ya 10 Mnigeria Samuel Peter mjini Frankfurt siku ya Jumamosi.

Haye alikuwa apambane na Klitscko mwezi wa Juni mwaka 2009 lakini badala yake akaamua kuzichapa na Nikolai Valuev mwezi wa Novemba ambapo alimchapa na kunyakua ubingwa wa uzito wa juu wa WBA.

Klitscko amesema:"Nimechoshwa na David Haye, tunamzungumzia sana. Natumai ataacha kuzungumza upuuzi na kutekeleza ahadi zake."

Haye siku za nyuma amekuwa akiwadhihaki akina Klitschko, ambapo aliwahi kuvaa fulana zenye picha ikimuonesha Haye amebeba vichwa vilivyokatwa vya Wladimir na kaka yake Vitali.

Wladimir ameongeza kusema:"David Haye amutudhihaki akina Klitschko wote wawili na haukuwa mzaha mzuri. Sidhani ilikuwa vyema kuonesha picha ya vichwa vyetu vimekatwa kwenye fulana, ambayo aliivaa kwenye mkutano na waandishi wa habari."

Iwapo Haye atagoma kupambana na Klitschko baada ya pambano lake na Harrison, mwalimu wa Klitschko Emanel Steward amesema bondia wake atapambana na bondia Mpoland anayeishi Marekani Tomasz Adamek.