X-ray yaonesha Walcott hajaumia sana

Theo Walcott
Image caption Theo Walcott

Mshambuliaji wa pembeni wa Arsenal na timu ya Taifa ya England, Theo Walcott ameumia kiwiko cha mguu wakati wa mchezo wa kutafuta nafasi ya kufuzu fainali za Kombe la Ulaya, England iliposhinda mabao 3-1 dhidi ya Switzerland.

Walcott mwenye umri wa mia 21 alitolewa uwanjani kwa machela baada ya kukwatuliwa na Yves Oehri wa katika heka heka za Rooney kupachika bao la kwanza dakika 10 ya mchezo.

Baadae alipelekwa hospitalini mjini Basle ambako alipigwa picha za x-ray katika mguu wake wa kuume.

Meneja wa England Fabio Capello ameelezea kuumia huko ni "tatizo dogo" lakini hakuweza kueleza tatizo lenyewe kwa undani.

Baada ya mechi, Capello alisema alizungumza na Theo na akamwambia si tatizo kubwa.

Nilimuuliza itachukua "wiki mbili", lakini Theo akasema ni chini ya hapo, aliongeza Capello.

Mchezo huo ulikuwa ni wa tatu wa kimataifa kwa Walcott kucheza tangu alipochujwa katika kikosi cha England kilichokwenda Afrika Kusini katika Kombe la Dunia.

Meneja wa Arsenal atakuwa anasubiri kwa hamu kujua tatizo la Walcott, mmoja wa washambuliaji anaowatumainia katika kikosi chake msimu huu.

Mapema siku ya Jumanne, Wenger alifahamishwa mshambuliaji wake Robin van Parsie hataweza kucheza kutokana na matatizo ya kuumia kiwiko cha mguu hadi katikati ya mwezi wa Oktoba.

Arsenal pia hadi sasa imekosa huduma ya mshambuliaji wake mwengine Nicklas Bendtner, ambaye anakabiliwa na matatizo ya nyonga, wakati kiungo hodari Samir Nasri anatazamiwa kuanza mazoezi siku chache zijazo baada ya kuwa nje ya uwanja tangu tarehe 15 mwezi wa Agosti alipoumia goti.