Capello kuondoka baada ya Euro 2012

Fabio Capello
Image caption Fabio Capello

Kocha wa England Fabio Capello amethibitisha atang'atuka baada ya kumalizika mashindano ya Euro mwaka 2012.

Baada ya kutofanya vizuri katika Kombe la Dunia mwaka 2010, hali iliyozua lawama kwa Capello, kwa sasa England inaongoza kundi G kwa ajili kufuzu mashindano ya Euro mwaka 2012.

Capello mwenye umri wa miaka 64 amejigamba:"Pasipo na shaka yoyote kwanza ni muhimu tufuzu, lakini baada ya hapo nitakuwa nimezeeka, kwa hiyo nataka kufurahia maisha yangu nikiwa nakula pensheni vizuri".

Capello alichukua nafasi ya Steve McClaren mwezi Desemba mwaka 2007.

Mshahara wake wa paundi milioni 6 kwa mwaka katika mkataba wake utampeleka hadi mwaka 2012.

Ameibadilisha England baada ya McClaren kushindwa kuifikisha hatua ya kufuzu katika mashindano ya Euro mwaka 2008, lakini baada ya kuonja upepo wa fainali za Kombe la Dunia, kikosi cha Capello kilisambaratishwa vibaya nchini Afrika Kusini na kutolewa katika mashindano ya Kombe la Dunia katika raundi ya pili baada ya kuchapwa mabao 4-1 na Ujerumani.

Wakati na baada ya fainali za Kombe la Dunia, Capello amekuwa akishutumiwa sana na vyombo vya habari kuhusiana na mbinu zake za utawala.

Hata hivyo, ameahidi kuendelea na kazi yake baada ya kuwepo fununu mkataba wake upo mashakani kabla ya Kombe la Dunia.

Katika heka heka za kufuzu kombe la Euro, England imeshazifunga Bulgaria na Switzerland hali iliyompunguzia hofu Capello, ambaye awali aliwahi kuzifundisha AC Milan, Roma, Juventus na Real Madrid.