Baada kuumia Defoe nje wiki sita

Jermain Defoe
Image caption Jermain Defoe

Mshambuliaji wa Tottenham Jermain Defoe, hataweza kucheza soka kwa muda wa wiki sita baada ya kuumia kiwiko cha mguu.

Defoe aliumia wakati England ilipowalaza Switzerland mabao 3-1 siku ya Jumanne na alitolewa nje kwa machela.

Kwa mujibu wa meneja wa Tottenham Harry Redknapp, hata kama tatizo ni kubwa, atakuwa nje kwa wiki sita au zaidi hali hiyo si nzuri.

Defoe atakosa michezo miwili ya Ubingwa wa Ulaya kwa klabu yake na kwa England hataweza kucheza mechi dhidi ya Montenegro ya kufuzu mashindano ya Euro mwaka 2012.

Kuumia kwa mshambuliaji huyo kumekuja wakati mbaya kutokana na kuonesha makali yake katika kupachika mabao, ambapo alifunga mabao 3 England ilipoitandika Bulgaria katika mchezo wa awali wa kampeni za Euro.

Pia inaonekana si bahati kwa klabu yake ya Tottenham na meneja wake Redknapp, kwa sababu mlinzi wa kati Michael Dawson naye hatacheza soka kwa wiki nane baada ya kuumia goti na kiwiko cha mguu, wakati England ilipocheza na Bulgaria katika uwanja wa Wembley.

Defoe alionekana akitumia magongo ya kutembelea huku akiwa amevaa kiatu maalum cha kinga siku ya Alhamisi katika uwanja wa mazoezi wa Tottenham.

Anatarajiwa kutocheza mechi tano za Ligi Kuu ya England na pia mechi ya Ubingwa wa Ulaya dhidi ya Werder Bremen na FC Twente.