Marekani yaonya mustakabali wa Mexico

Tukio la mashambulizi ya magenge ya mihadarati

Mexico imepinga matamshi ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hilary Clinton, kwamba baadhi ya magenge ya wafanyi biashara ya mihadarati wamekuwa wakiendesha kile alichokiita maasi nchini Mexico.

Msemaji wa serikali ya Mexico Alejandro Poire amepinga tamko la Bi Clinton ambapo alifafanisha hali ya Mexico na Colombia miaka 20 iliyopita ambapo walanguzi wa mihadarati walithibiti maeneo mengi ya nchi.

Afisa huyo amesema machafuko yanayokumba Mexico na Colombia yamesababishwa na soko la mihadarati huko Marekani.Matamshi ya Clinto yametokea wakati likitolewa onyo la usalama kutokana na harakati za magenge ya mihadarati.

Zaidi ya watu elfu 20 wamekufa kwenye machafuko kati ya magenge ya mihadarati, nchini Mexico tangu rais Felipe Calderon kushirikisha jeshi kukabiliana na magenge hayo mwaka 2006.

Huku haya yakiarifiwa maafisa wa Mexico wamedhibitisha kukamatwa kwa watu saba wanapshukiwa kuhusika na mauaji ya wahamiaji 72. Magenge ya mihadarati yamelaumiwa kuhusika na mauaji hayo.

Msemaji wa serikali amesema wanajeshi wa Mexico waliwakamata watu wanne wiki moja iliyopita na wengine kutiwa mbaroni baadaye.

Miili ya wahamiaji hao kutoka nchi za Amerika ya Kati ilipatikana mwezi jana na wanajeshi wa Mexico kwenye uwanda mmoja kaskazini mwa jimbo la Tamaulipas baada ya kutokea ufyatulianji wa risasi na makundi ya mihadarati.