Rais wa Nigeria afanyia mabadiliko idara za usalama

ramani ya  Nigeria

Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, amewateua wakuu wapya wa jeshi, idara ya upelelezi na polisi saa chache baada ya kuwafuta kazi walioshikilia nyadhifa hizo.

Hatua hiyo inakuja baada ya gereza moja lililoko Kaskazini mwa nchi hiyo kushambuliwa na wanachama wa kundi la kiislamu nchini humo, na kusababisha wafungwa mia saba kutoroka.

Hakuna sababu iliyotolewa kwa hatua hiyo lakini taarifa kutoka ikulu ya Rais iliwashukuru wakuu hao kwa huduma zao kwa raia.

Wengi wanaitafsiri hatua hii kuwa ya kisiasa ili kuhakikisha kwamba maafisa wa jeshi na wale wanaohudumu katika idara za usalama wanamtii rais Goodluck Jonathan. Rais Jonathan bado hajatangaza iwapo atawania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu unaopangwa kufanyika Januari, mwaka ujao.

Hata hivyo wengi wanatarajia kuwa atawania kiti hicho na atatoa tangazo hilo hivi karibuni. Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema huu ni wakati muhimu sana kisiasa kwa rais Goodluck Jonathan, wakisema kuwa jeshi pamoja na maafisa wa usalama watakuwa wakishughulikia mabadiliko ambayo yametokea na hivyo hawatakuwa makini wakati wa kipindi hiki muhimu. Lakini rais Goodluck Jonathan ana maadui katika serikali yake ambao hawataki awanie kiti hicho. Jonathan alichukua wadhifa huo baada ya kifo cha mtangulizi wake, Umaru Yar'Adua, kufariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu. Rais Yar'Adua alitoka eneo la Kaskazini mwa nchi hiyo. Wengi walidhania kwamba kufuatia kifo cha rais Yar'Adua mtu ambaye angefaa kumrithi angetoka eneo hilo la Kaskazini, lakini haikuwa hivyo. Goodluck Jonathan anatoka kusini mwa Nigeria. Nigeria ina raslimali nyingi za mafuta na hatua ya rais Jonathan inaonekana na baadhi ya watu kama njia moja ya kuhakikisha anabakia na ushawishi katika taasisi muhimu za nchi hiyo.