Ni kiwewe ikiwa kasisi mmoja atachoma Quran

Nakala za Quran

Kasisi wa Kimarekani ambaye amezua lalama kali duniani kufuatia mpango wake wa kuchoma Koran tukufu hapo Kesho Septemba 11 amesema mpango wake utategemea kutekelezwa kwa masharti anayotaka yafanywe.

Saa chache zilizopita, Mchungaji Terry Jones alitangaza kufutilia mbali mpango wake wa kuchoma moto nakala za Koran tukufu

Hii ilikuwa baada ya kudai kwamba alikuwa amefikia makubaliano na viongozi wa kiislamu.Alidai walikubaliana kubadili sehemu ya kujenga kituo cha kiislamu, mjini New York, ili naye mchungaji huyo afutilie mbali uamuzi wake wa kuchoma moto nakala za kitabu cha Koran.

Jones aliandamana na Imam wa eneo lake akitoa tangazo hilo.

"Raia wa Marekani hawataki msikiti pale na bila shaka waislamu hawataki sisi tuchome Koran. Imam amekubali kuhamisha mpango wa kujenga kituo cha utamaduni cha kiislamu, katika eneo ambako mashambulio yalifanyika"Alisema Jones.

Hata hivyo si wazi kama makubaliano yamefikiwa. Msemaji wa kundi linalohusika na ujenzi wa kituo hicho amesema kuwa hakuna mpango wowote wa kuhamisha kituo hicho na msikiti.

Bw Jones anadai kuwa viongozi hao wa kiislamu walimhadaa.

Huenda kile mchungaji Jones anachosema ni makubaliano, ni mazungumzo tu kwamba yeye na Imam wa New York, Faizal Rauf, ambaye ndiye msimamizi wa mradi huo watakutana jumamosi kujadili, hali ambayo bado ni ya utata kuhusu ujenzi wa kituo hicho.

Awali, katika mohojiano na kituo cha televisheni cha ABC, rais Obama alitaja mpango wa mchungaji huyo kama mchezo wa kuigiza.

"Kama anasikiliza natumaini anaelewa kwamba kile anachopendekeza kukifanya, ni kinyuma kabisa na maadili yetu kama wamarekani. Kwamba nchi hii ilijengwa kwa misingi ya uhuru wa kuabudu na kuvumiliana kwa dini. "alionya Obama.

Kitendo cha mchungaji huyo kutaka kuchoma moto kitabu cha Koran kimeshutumiwa vikali kote duniani.