Marekani yaadhimisha mashambulizi ya 9/11

Waandamanaji mjini New York
Image caption Waandamanaji mjini New York

Saa chache baada ya sherehe kufanyika nchini Marekani kuadhimisha miaka tisa ya mashambulizi ya September 11, makundi mawili ya waandamanaji yanayotofautiana yameandamana kati kati ya mji wa New York.

Kundi moja linaunga mkono ujenzi wa kituo cha kiislam karibu na jengo la World Trade Centre lililoangushwa wakati wa mashambulizi ya mwaka wa 2001, huku lingine likipinga mpango huo.

Mamia ya watu wanaounga mkono ujenzi wa kituo hicho wamekuwa wakibeba mabango yanayotoa wito wa kudumishwa kwa uvumilivu na kumalizwa kwa tabia ya kuchukia Uislamu.

Kiasi cha masafa ya mita mia tatu kutoka eneo la maandamano ya wanaounga mkono mpango huo, mamia ya watu wengine wamekusanyika kupinga wazo hilo la ujenzi wa kituo cha kiislam.

Mwandishi wa BBC mjini New York amesema idadi kubwa ya polisi walikuwa katika eneo la maandamano kwa vile wakati fulani waandamanaji wamekuwa wakizidiwa nguvu na hasira.

Akizungumza katika makao makuu ya wizara ya ulinzi ya Marekani ya Pentagon mjini Washington, ambayo pia ilishambuliwa mwaka wa 2001, Rais Obama alisema Wamarekani hawakuwa na kamwe hawatokuwa vitani na Uislam,bali wako vitani na kundi la Al Qaeda.