Marekani kuadhimisha mashambulizi ya 9/11

Maadhimisho ya mashambulizi ya Sept 11
Image caption Maadhimisho ya mashambulizi ya Sept 11

Sherehe zitafanyika leo nchini Marekani kuadhimisha mashambulizi ya Septemba kumi na moja miaka tisa iliyopita, ambapo watu karibu elfu tatu waliuwawa.

Maadhimisho ya mwaka huu yamegubikwa na utata unaondelea juu ya mipango ya kujenga kituo ca kiislam karibu na viwanja vya mashambulizi hayo mjini New York, na tishio, ambalo sasa limesitishwa, la kasisi wa kanisa moja ndogo katika jimbo la Florida kutaka kuchoma moto nakala za kitabu cha Koran.

Mwandishi wa BBC mjini New York amesema maadhimisho ambayo kwa kawaida hufanyika kwa huzuni mwaka huu yanaelekea kuwa yenye utata mkubwa, pamoja na maandamano ya kuunga mkono na yenye kupinga ujenzi wa kituo cha kiislam yatakayoanza punde baada ya maadhimisho kumalizika.

Obama akemea mpango wa kuchoma Koran

Rais Obama ametoa wito kwa Wamarekani kudumisha heshima kwa imani za kidini za watu wengine, wakati mataifa ya Kiislam yakionyesha upinzani mkali juu ya tishio la kanisa dogo la Kimarekani kutaka kuchoma moto kitabu cha Koran.

Bw Obama alisema kuchoma maandishi ya kidini ni kinyume na maadili mema ambayo ndiyo msingi wa Marekani.

Kasisi anayetaka kutekeleza kitendo hicho, Terry Jones, amesema amesitisha mpango wake wa kuchoma Koran wakati wa maadhimisho ya mashambulizi ya Septemba kumi na moja , lakini anataka kukutana na Imam anayesimamia mpango wa kutaka kujenga kituo cha kiislam karibu na eneo la jengo lililoangushwa katika mashambulizi hayo la World Trade centre mjini New York.