Zambia yakanusha maovu katika magereza yake

Waziri wa zamani wa Zambia akiwa jela
Image caption Waziri wa zamani wa Zambia akiwa jela

Serikali ya Zambia imekanusha taarifa kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na mateso katika magereza nchini humo.

Waziri wa mambo ya ndani Mkhondo Lungu alisema katika taarifa rasmi kuwa Zambia ilitia saini mikataba kadhaa ya kimataifa juu ya haki za binadamu, na maafisa wa serikali waliagizwa kuwatunza washukiwa kwa misingi ya kibinadamu.

Pia Waziri Lungu alisema serikali inafanya juhudi za kuimarisha mazingira ya magereza yake kote nchini.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lenye makao yake mjini New York katika repoti yake iliyochapishwa siku ya Jumanne ilidai kuwepo kwa ukiukwaji wa haki za wafungwa katika magereza sita nchini Zambia.

Human Rights Watch katika repoti yake ilisena imepata ushahidi kutoka kwa wafungwa waliosema walipigwa kwa nondo, nyundo na chuma chenye nguvu za umeme.