FA kumshitaki meneja wa Everton

David Moyes
Image caption David Moyes

David Moyes anakabiliwa na mashtaka ya mwenendo mbaya baada ya kumkabili na kumfokea mwamuzi Martin Atkinson kufuatia matokeo ya sare ya mabao 3-3 katika mchezo baina ya Everton na Manchester United siku ya Jumamosi.

Msaidizi wa Moyes, Steve Round pia anakabiliwa na mashtaka kutoka chama cha soka cha England (FA) na wote wawili wametakiwa hadi siku ya Alhamisi kujibu mashtaka yao.

Chini ya sheria mpya za FA za kushughulikia masuala kwa haraka, iwapo watakiri mashtaka watawajibika kulipa paundi za Uingereza 8,000.

Hata hivyo iwapo watakana mashtaka, shauri lao litaahirishwa na kuzungumzwa ndani ya siku 10.

Everton ilifanikiwa kufunga mabao mawili ndani ya dakika za nyongeza, lakini Moyes hakufurahishwa na mwamuzi Atkinson hakuruhusu muda zaidi wa mchezo.

Meneja huyo wa Everton amesema hilo lilikuwa ni kosa kubwa kwa uamuzi wa Atkinson. Meneja huyo alivamia uwanja baada ya mchezo kumalizika kumkabili Atkison na kuonekana akimfokea mwamuzi.