Rooney ajifua kuikabili Rangers

Wayne Rooney
Image caption Wayne Rooney

Mshambuliaji wa Manchester United Wayne Rooney amefanya mazoezi Jumatatu asubuhi kwa maandalizi ya pambano la Ubingwa wa Ulaya dhidi ya klabu ya Rangers ya Scotland siku ya Jumanne.

Rooney aliondolewa katika kikosi cha Manchester United kilichopambana na Everton, huku Sir Alex Ferguson akidai hakumchezesha kwa ajili ya kumlinda dhidi ya kashfa kutoka kwa mashabiki wa Everton ambayo ni klabu yake ya zamani.

Taarifa za magazeti zimekuwa zikiandika mshambuliaji huyo alikuwa akiwalipa makahaba kwa ajili ya kufanya nao mapenzi.

Rooney alionekana akicheka na kufanyiana mzaha na wachezaji wenzake katika uwanja wa mazoezi wa Carrington mjini Manchester.

Mshambuliaji huyo anatazamiwa kuanza katika mchezo wa siku ya Jumanne, wakati United itakapotaka kurekebisha makosa yake kutokana na kunyang'anywa tonge la pointi tatu mdomoni, walipofungwa mabao mawili dakika za mwisho walipocheza na Everton.

Man U walifungwa mabao hayo wakati wa dakika za nyongeza na kupoteza pointi tatu muhimu.

Hadi sasa United wapo nafasi ya tatu nyuma ya vinara wa Ligi Kuu ya soka ya England, Chelsea kwa pointi nne na Arsenal.

Hata hivyo kwa sasa United imeelekeza nguvu katika mashindano ya Ulaya na zaidi pambano dhidi ya Rangers, ikiwa ni mechi yao ya kwanza ya kuwania Ubingwa wa Ulaya msimu huu, ambapo pia kundi lao zimo timu za Valencia ya Hispania na Bursaspor ya Uturuki.