TP Mazembe yachukia kufungiwa wachezaji

Tresor Mputu
Image caption Tresor Mputu

Rais wa TP Mazembe Moise Katumbi amechukizwa na uamuzi wa kuwafungia wachezaji wawili muhimu wa klabu hiyo.

Hasira zake zimekuja muda mfupi baada ya TP Mazembe kufuzu kucheza nusu fainali ya ubingwa wa vilabu vya Afrika kwa mwaka 2010.

Klabu hiyo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, kwa kufuzu huko imengia hatua ngumu ya mashindano hayo bila nahodha wake Tresor Mputu na kiungo Guy Lusadisu.

Fifa imemfungia kucheza soka mwaka mmoja Tresor Mputu na miezi 11 kwa Lisadisu, kutokana na wachezaji hao kushiriki katika vurugu wakati wa mashindano ya Cecafa mwezi Mei nchini Rwanda.

TP Mazembe katika mshindano hayo ilialikwa tu, lakini ikaondolewa baada ya mechi dhidi ya wenyeji APR kusimamishwa.

Mputu na Lusadisu wameonekana ndio vinara wa ghasia hizo zilizosababisha wachezaji kurushiana ngumi, hali iliyosababisha mwamuzi kusimamisha mchezo.

Nahodha huyo wa TP Mazembe alitolewa nje baada ya kupandwa hasira na kumshambulia mwamuzi, wakati Lusadisu alimpiga afisa usalama aliyeingia uwanjani kujaribu kutuliza ghasia hizo.

Lakini Katumbi amepinga ukubwa wa adhabu zilizotolewa na kusema ni kali kwani wachezaji hao hawataiwakilisha klabu yao kwa muda mrefu.

Katumbi amesema wanaiomba radhi Cecafa na amepokea barua kutoka Shirikisho hilo ikikubali msamaha wao.

Rais huyo wa TP Mazembe amesema anaamini wachezaji wake wanajutia makosa waliyotenda kutokana na adhabu waliyopewa katika ngazi ya eneo lao, akaongeza anataka kufahamu namna uamuzi wa kuwafungia wachezaji wake ulivyofikiwa.