Valencia kutocheza msimu mzima

Antonio Valencia
Image caption Antonio Valencia

Mshambuliaji wa pembeni wa Manchester United Antonio Valencia huenda asiweze kucheza msimu huu mzima baada ya kuumia vibaya kiwiko cha mguu wakati wa mchezo wa Ubingwa wa Ulaya dhidi ya Rangers siku ya Jumanne.

Valencia alitolewa nje kwa machela baada ya kunguka akionekana mwenye maumivu makali baada ya kukabiliwa na Kirk Broadfoot katika dakika ya 62.

Winga huyo mwenye umri wa miaka 25 alipelekwa hospitali na amefanyiwa upasuaji.

Kwa mujibu wa meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, inaonekana amevunjika na hali hiyo itamfanya asicheze msimu mzima.

Ferguson amelinganisha kiwango cha kuumia kwa Valencia sawa na alivyowahi kuumia mchezaji wa zamani wa Manchester United Alan Smith, aliyevunjika mguu wa kushoto na kiwiko cha mguu kikatoka kwenye mchezo wa kombe la FA mwezi Februari mwaka 2006 dhidi ya Liverpool.

Smith kutokana na kuumia huko hakucheza soka kwa muda wa miezi saba na iwapo kama hali hiyo itakuwa sawa na ya Valencia, mchezaji huyo ataweza kurejea dimbani mwezi Aprili mwaka 2011.

Broadfoot ambaye haraka alionekana akiashiria Valencia anahitaji huduma ya haraka, akizungumza baada ya mchezo huo, alisema alipata woga kuangalia namna Valencia alivyoumia.