Henry asema hakukusudia kumvunja Zamora

Bobby Zamora
Image caption Bobby Zamora

Nahodha wa Wolves Karl Henry amekanusha madai kwamba alijaribu kumuumiza kwa makusudi Bobby Zamora baada ya mshambuliaji huyo wa Fulham kuvunjika mguu siku ya Jumamosi.

Upasuaji aliofanyiwa Zamora umeonesha mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29, pia ameumia kiwiko cha mguu na anatazamiwa kuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha miezi minne.

Mwamuzi Phil Dowd hakupuliza filimbi kutokana na rafu hiyo na Henry kupitia mtandao wa Wolves amesema: "Nilihisi nilimkabili pasipo kumchezea rafu."

Ameongeza kusema: "Sikufanya rafu ya makusudi na kamwe sitajaribu kumuumiza mchezaji yeyote. Naomba radhi Zamora ameumia."

Fulham ilishinda kwa mabao 2-1 kwa bao la ushindi lililofungwa dakika za nyongeza na Moussa Dembele, lakini ushindi huo uligubikwa na kuumia kwa Bobby Zamora katika kipindi cha kwanza , ambaye ni hivi karibuni tu alipona matatizo ya paja na alikuwa akicheza mchezo wake wa kwanza tangu alipotia saini mkataba mpya wa miaka minne kuichezea Fulham.