Wamarekani 4 wakamatwa Zimbabwe

Maafisa wa polisi nchini Zimbabwe wamewakamata wafanyikazi wanne wa afya kutoka Marekani.

Image caption Wafanyikazi wa afya kutoka Marekani inadaiwa hawana leseni wala idhini ya kutoa dawa

Kulingana na ubalozi wa Marekani mjini Harare, wafanyikazi hao ambao wamekuwa wakitoa misaada ya kupambana na ukimwi, inadaiwa wamekuwa wakiendesha kliniki moja ya kutoa dawa na misaada, na ambayo haijasajiliwa, wala kuwa na kibali cha kufanya hivyo.

Watu wawili wengine wenye uraia wa Zimbabwe pia wanazuiliwa.

Kulingana na taarifa ya ubalozi wa Marekani, wote sita wanatazamiwa kufikishwa mahakamani Jumatatu.

Kundi hilo la matabibu, ambalo lilikuwa likiendesha shughuli zake katika kliniki mbili, mjini Mutoko na Harare, limekanusha madai hayo.

Katika kundi hilo la Kikristomisaada kutoka California, lina daktari mmoja, wauguzi wawili, na mfanyikazi mmoja wa huduma za jamii.

Kazi yao hasa imekuwa ni kuwatunza watoto mayatima, waliofiwa na wazazi waliokuwa na Ukimwi ama wenye virusi vya HIV.

Msemaji wa polisi, alilielezea gazeti linalosimamiwa na serikali la Herald, kwamba watu hao sita wanazuiliwa "ili kuhojiwa kwa kuendesha kazi pasipo kuwa na leseni ya wanapofanyia kazi, na kutoa dawa pasipo kuwa na afisa anayesimamia dawa".

Wafanyikazi hao ni wafuasi wa kanisa la Baptist huko Oakland, Marekani.

Mhubiri kutoka kanisa hilo, Teophous Reagans, aliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba wafanyikazi hao wa kujitolea ni waumini wa kanisa hilo, na wamekuwa wakitoa huduma nchini Zimbabwe katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.