Mashabiki Liverpool wakasirishwa na timu

Mashabiki wa Liverpool
Image caption Mashabiki wa Liverpool

Meneja wa Liverpool Roy Hodgson amesema "hawezi kuwalaumu" mashabiki walioendesha upinzani dhidi ya wamiliki wa klabu baada ya timu hiyo kwenda sare ya mabao 2-2 na Sunderland.

Amesema: "Sitazamii mtu yeyote ndani ya klabu anahitaji kitu kingine zaidi ya usuluhishi kutokana na matatizo ya umiliki."

Mashabiki wanataka kuona klabu yao inasonga mbele na kumaliza matatizo ya wamiliki wanaotaka kuuza klabu.

Mashabiki takriban ya 10,000 walibakia uwanja wa Anfield baada ya mchezo kumalizika wakihoji mipango ya wamiliki wawili wa klabu hiyo George Gillett na Tom Hicks ya kuuza klabu hiyo.

Benki ya RBS, inayoidai klabu hiyo paundi milioni 237 katika deni la Liverpool la paundi milioni 282, wanasubiriwa kusema chochote juu ya deni lao mwezi wa Oktoba.

Benki hiyo inayomilikiwa kwa asilimia 84 na serikali, huenda ikaamua kumiliki kampuni ya Kop Holdings, iliyotumiwa na Hicks pamoja na Gillett mwezi wa Februari mwaka 2007 kuinunua Liverpool.

Wamiliki hao inasemekana wanataka paundi milioni 600 kuiuza klabu hiyo, huku paundi milioni 420 wakizipata watakuwa wameiuza klabu kwa hasara.

Hata hivyo iwapo klabu ya Liverpool itaangukia mikononi mwa umiliki wa benki, inaweza kuuzwa kwa paundi milioni 280, ikiwa ni pamoja na adhabu ya paundi milioni 40.

Meneja wa Liverpool Hodgson yupo katika heka heka kubwa za kuhakikisha klabu hiyo inafanya vizuri tofauti na msimu uliopita ilipomaliza nafasi ya saba katika ligi.

Hadi sasa Liverpool imeshinda mchezo mmoja tu kati ya sita ya ligi msimu huu na walitolewa katika mbio za kuwania kombe la Carling nyumbani kwao walipofungwa na Northampton ya daraja la pili hivi karibuni.