Spurs yaangushiwa kichapo kizito

Harry Redknapp
Image caption Harry Redknapp

Meneja wa Tottenham Harry Redknapp amemsutumu Samir Nasri kwa kujiangusha baada ya kiungo huyo wa Arsenal kufanikiwa kupata mkwaju wa penalti ulioisaidia timu yake kuichabanga mabao 4-1 na kuitoa Spurs katika mashindano ya Kombe la Carling.

Nasri alifunga mkwaju huo wa penalti na baada ya muda mfupi akafunga bao jingine kwa mkwaju wa penalti, kabla Andrey Arshavin kukufunga kitabu cha mabao.

Lakini Redknapp alihamaki na kusema: "Nadhani penalti ya kwanza haikuwa halali. Alijiangusha makusudi."

Akaongeza: Lakini niliona mchezo ungekuwa mgumu kwa upande wetu kutokana na mchezo wa Arsenal, walionekana kutuzidi kila idara."

Image caption Samir Nasri

Arsenal iliandika bao la kwanza baada ya Henri Lansbury kuunganisha krosi safi, kabla Robbie Keane kusawazisha katika kipindi cha pili, lakini mikwaju miwili ya penalti ya Nasri, na bao la nne la Arshavin ilitosha kuwatoa Spurs katika kuwania kombe la Carling.

Gunners walimiliki mchezo kwa muda mwingi licha ya meneja wake Arsene Wenger kutokuwepo kwenye benchi la ufundi kutokana na kutumikia adhabu ya mechi moja baada ya kumzonga mwamuzi wa akiba wakati wa mchezo wa ligi na Sunderland siku ya Jumamosi.

Wenger alionekana kufurahishwa na kiwango cha soka kilichooneshwa na vijana wake na kuelekeza sifa kemkem kwa Jack Wilshere kiungo mwenye umri wa miaka 18 aliyekuwa akitawala sehemu ya katikati ya uwanja kwa ustadi mkubwa.