Obama ashinikiza kura ya haki Sudan

Image caption Rais wa Sudan Omar al-Bashir

Rais wa Marekani Barack Obama anatarajiwa kuhudhuria mkutano maalum wa Umoja wa Mataifa kushinikiza maafisa wa Sudan kuhakikisha kura ya maoni ya mwezi Januari iwe huru na ya haki.

Sudan Kusini inatarajiwa kupiga kura ya kuamua iwapo eneo hilo lijitawale lenyewe au la.

Lakini maandalizi yanaonekana bado hayajakamilika, huku serikali mpaka sasa ikiwa haijaamua nani wa kupiga kura.

Upande wa Kusini unasisitiza kura hiyo ipigwe kwa wakati uliopangwa, na usiahirishwe.

Kura hiyo ya maoni ni sehemu ya makubaliano ya amani ya mwaka 2005 ya kumaliza miongo miwili ya mapigano baina ya upande wa kaskazini na upande wa kusini wenye utajiri wa mafuta, lakini waangalizi wanahofia ucheleweshaji au ukosefu wa kura zenye kuaminika unaweza kuchochea mgogoro upya.

'Hatari ya kulipuka'

Image caption Slav Kiir

Mwandishi wa BBC James Copnall aliyopo mjini Khartoum alisema kunahitajika azma ya kweli ya kisiasa, vile vile vifaa vya kutosha, ili kuweza kupiga kura hiyo kwa muda unaotakiwa - lakini mpaka sasa, vyote hivyo havipo.

Mwandishi wetu alisema, huu ni mkutano wa Umoja wa Mataifa, lakini bila ya shaka kuwepo kwa Bw Obama ni muhimu.

Rais wa Sudan Omar al-Bashir amerudia mara kwa mara akisema kura hiyo itakuwa huru na ya haki, lakini wakosoaji hawaamini, na baadhi wanamshutumu kwa kuisogeza mbele kusudi.

Bw Bashir, anayetakiwa na umoja huo kwa makosa ya uhalifu wa kivita, anawakilishwa na makamu wake Ali Osman Taha, huku Sudan Kusini ikiwakilishwa na kiongozi wake Salva Kiir.

Mapema mwezi huu, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton aliita kura hiyo ya Januari 9 "bomu linalokaribia kulipuka'.

Alionyesha wasiwasi kuwa upande wa kaskazini si rahisi kukubali kupoteza nafasi yake ya kugawana mapato ya mafuta na upande wa kaskazini ujitahidi kuwapa nafasi hiyo, ili kuzuia mapigano kujirudia.

Sudan Kusini, ambapo wengi ni Wakristo au hufuata imani za kiutamaduni, tayari inajitawala kwa kiasi fulani na inaongozwa na waliokuwa waasi wa SPLA, waliopigana na wengi ambao ni waislamu, wanaozungumza kiarabu upande wa kaskazini mpaka makubaliano yalipofikiwa mwaka 2005.