Keegan amshambulia Rooney

Kevin Keegan
Image caption Kevin Keegan

Meneja wa zamani wa England Kevin Keegan, amesema Wayne Rooney asivilaumu sana vyombo vya habari kutokana na kushuka kiwango chake cha usakataji soka kwa klabu yake ya Manchester United.

Rooney mwenye umri wa miaka 24 amekuwa akibebeshwa lawama nyingi kuhusiana na maisha yake binafsi, amefunga bao moja tu katika michezo sita Manchester United iliyocheza msimu huu.

Na Keegan anaamini aina ya maisha aliyochagua kuishi Rooney hayakumsaidia.

Keegan ameongeza kusema: "Huwezi kuanza kusema kumekuwa na mapaparazi wengi au vyombe vya habari vimemuandika sana."

"Huwezi kuwa na mawasiliano ya watu wote, ukauza haki ya harusi yako kwa magazeti na mambo mengine kama hayo na ghafla unageuka na kusema, hilo ndio bomba ninalotaka kulifungua lakini jingine tulifunge."

Ameongeza kusema Keegan:"Ni bomba moja tu na kadri ninavyofahamu enzi zangu za uchezaji soka, iwapo unatangaza viatu vya mpira na vitu vinavyofanana na hivyo, unatakiwa kujitokeza. Ni lazima uonekane magazetini.

Lakini Keegan akamuasa Rooney ni vyema kuiepusha nyumba na familia yake na mambo hayo na atafute ushauri iwapo anataka kuendelea na maisha kama hayo.

Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson amesema Rooney amekuwa akikabiliwa na maudhi yanayoandikwa na vyombo vya habari kumhusu yeye na kwa mara nyingine hakucheza vizuri siku ya Jumapili walipotoka sare ya mabao 2-2 na Bolton katika uwanja wa Reebok.

Rooney alitolewa na nafasi yake ikachukuliwa na Federico Macheda katika dakika ya 61, ingawa mshambuliaji huyo wa zamani wa Everton baadae alionekana kufunga mguuni mfuko uliojaa barafu.

Lakini meneja msaidiza wa Manchester United Mike Phelan, amesema mshambuliaji huyo atakuwa tayari kucheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya siku ya Jumatano dhidi ya Valencia.