Mshindi wa tuzo ya Nobel aanzisha chama

Image caption Wole Soyinka

Mshindi wa tuzo ya Nobel ya fasihi Wole Soyinka amezindua chama cha kisiasa nchini Nigeria, miezi michache kabla ya uchaguzi wa Rais kufanyika.

Alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama cha The Democratic Front for a People's Federation katika sherehe mjini Lagos.

Chama hicho kipya kimesema kina nia ya kupambana na rushwa na kuimarisha masuala ya afya na elimu Nigeria.

Vitabu na maigizo ya Wole Soyinka imetambulika duniani kote, lakini pia anajulikana kama mwanaharakati wa kisiasa.

Kitabu chake cha "The Man Died" cha mwaka 1972 kilihusu muda wake aliyokaa gerezani wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Nigeria kuanzia mwaka 1967-70.

Alikuwa Mwafrika wa kwanza kupewa tuzo ya Nobel ya fasihi mwaka 1986.

Uchaguzi wa Rais na wabunge unatarajiwa kufanyika mwakani lakini haijajulikana iwapo Bw Soyinka ana nia ya kugombea.